Matukio

Habari

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kulipa fidia wakazi wa Mbagala

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kulipa fidia wakazi wa Mbagala

Wakati Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ukiwa katika maandalizi ya mwisho ya kuanza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya 2 ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopaswa kupisha ujenzi wa miundombinu hiyo imeanza.

Kuanza kwa zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi husika kumebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji wa DART Bw. Victor Ndonne wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi wa utaratibu wa ulipaji wa fidia hiyo kwa wananchi walioanishwa katika Jedwali la Fidia katika Awamu ya 2 ya mradi wa DART.

Bw. Victor Ndonne alitoa ufafanuzi katika kikao ambacho kilijumuisha maafisa kutoka DART, Manispaa ya Temeke na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kuwa Awamu ya 2 ya Mradi ni miongoni mwa Awamu 6 zinazotarajiwa kutekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam zinazozihusu Barabara za Nyerere hadi Gongo la Mboto, Barabara ya Kawawa hadi Tegeta, Barabara ya Mandela na Barabara ya Mwai Kibaki.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kazi ya uthamini na uhakiki wa Majedwali ya Fidia kwa ajili ya wananchi wenye majengo yanayopaswa kupisha ujenzi wa Awamu ya 2 ya Mradi huo imekamilika na tayari majedwali hayo yalikabidhiwa kwa Wakala kwa ajili ya ulipaji wa fidia.

Alibainisha maeneo ambayo wananchi wangelipwa fidia ni pamoja na Mbagala Rangi tatu katika Mtaa wa Mianzini, Misheni na Keko. Aidha, aliendelea kueleza kuwa katika malipo ya fidia hiyo zipo taasisi za Serikali ambazo zinapaswa kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa miundo mbinu hiyo. Taasisi hizo ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Walimu (DUCE).

Aliendelea kueleza kuwa ulipaji wa fidia hiyo utajumuisha wananchi 71 kutoka katika Mtaa wa Mianzini, Wananchi 15 katika eneo la Viwanda la Mbagala Rangitatu, Wananchi 10 kutoka Kata ya Keko, wananchi 6 kutoka Mtaa wa Misheni pamoja na taasisi 2 zilizotajwa hapo juu. Aidha, ilielezwa kuwa yapo makaburi yasiyopungua 100 katika Mtaa wa Mianzini ambayo pia yatapaswa kuhamishiwa katika maeneo mengine ili kupisha Mradi huu.

Baada ya ufafanuzi uliotolewa, Mkurugenzi huyo alihimiza wananchi watakaokuwa wamelipwa fidia kujiandaa mapema kuhama ili kupisha ujenzi wa miundombinu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Alieleza kuwa tayari mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu hiyo amepatikana na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza mara moja.


Ramani

    Hakuna Taarifa kwa sasa