Chalamila auhakikishia umma kuimarika kwa huduma za BRT kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amezungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, uliolenga kuelezea hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma za usafiri kupitia mfumo wa BRT.
Mkutano huo umehudhuriwa na waandishi wa habari zaidi ya 100 kutoka vyombo mbalimbali vya habari wenye lengo la kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto zinazojitokeza kwa sasa katika uendeshaji wa huduma za mabasi chini ya Mtoa Huduma wa Mpito (TSP), ambaye ni UDART.
Akizungumza na wanahabari, RC Chalamila amesisitiza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imejipanga kuimarisha mfumo wa usafiri wa BRT kwa kutumia mbinu ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) badala ya kutegemea taasisi za serikali peke yake.
Ameleeza kuwa mbinu hiyo mpya tayari imeanza kuzaa matunda, ambapo Wakala wa DART umefanikiwa kutangaza zabuni na kupata Watoa Huduma kwa Awamu ya Kwanza na ya Pili, ambazo zinahusisha barabara ya Morogoro na barabara ya Kilwa.
“Kwa kutumia PPP, tumepata wawekezaji binafsi. Kampuni ya TransDar, ambayo ni Mtoa Huduma kwa Awamu ya Kwanza, italeta mabasi 177 ya kisasa yanayotumia dizeli ya kiwango cha Euro 6, ambayo yataanza kutoa huduma Oktoba 2025,” amesema RC Chalamila.
Kwa upande wa Awamu ya Pili, ambayo itaanza Agosti 2025, RC ameeleza kuwa kampuni ya Mofat Company Limited imepangwa kutoa huduma kwenye njia kuu kwa kutumia mabasi 200 yanayotumia gesi asilia iliyoshindikizwa (CNG), kwa lengo la kulinda mazingira.
“Aidha, kampuni nyingine mbili zimepangwa kutoa huduma katika njia za mlisho za Awamu ya Pili, na kufanya jumla ya mabasi kuwa 700. Hii itaongeza sana upatikanaji wa mabasi na kupunguza msongamano,” ameongeza kusema.
RC Chalamila amebainisha kuwa matumizi ya gesi na dizeli ya Euro 6 ni mkakati wa makusudi unaolenga kupunguza uchafuzi wa hewa na kuimarisha usafiri wa kijani jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa changamoto zilizopo kwa UDART ni za muda mfupi na Serikali iko makini katika kuhakikisha mabadiliko haya mapya yanazaa matokeo ya muda mrefu kwa wananchi.
Pia ameipongeza DART kwa hatua zake za kimkakati, zikiwemo kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kupata Watoa Huduma kwa Awamu ya Tatu na ya Nne.
“Kwa njia hii, mara tu ujenzi wa miundombinu utakapokamilika, tayari Watoa Huduma watakuwa wamepatikana na wako tayari kuanza kazi bila kuchelewa,” amesema Chalamila.
Amewataka wananchi kuwa na subira na kuunga mkono jitihada hizi kwani maboresho makubwa ya usafiri yataonekana mara tu mabasi mapya yatakapoanza kazi.
Aidha, ameisifu DART kwa usimamizi bora, uwazi, na mawasiliano mazuri katika mchakato wa PPP na ushirikiano wake na washirika wa kimataifa kama IFC.
Akizungumza katika mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Dkt. Athumani Kihamia, amethibitisha kuwa Wakala uko tayari kusimamia kwa ufanisi huduma za usafiri pindi Watoa Huduma wapya watakapoanza rasmi.