DART yatembelea Lake Oil kukagua maandalizi ya gesi asilia (CNG) kwa awamu ya Pili

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dkt. Athumani Kihamia, ameongoza ujumbe wa Menejimenti na maafisa wengine wa Wakala huo kutembelea ofisi za kampuni ya Lake Oil kufuatilia maendeleo ya maandalizi ya kusambaza Gesi Asilia (CNG) kwa ajili ya mabasi ya Awamu ya Pili.
Lake Oil ndiyo kampuni iliyosaini mkataba wa kusambaza gesi ya CNG katika mfumo wa DART Awamu ya Pili, unaopita barabara ya Kilwa hadi Mbagala. Ziara hiyo imekuwa ni sehemu ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa vituo vya kujaza gesi hiyo katika karakana ya Mbagala na maeneo mengine ya mfumo wa BRT awamu ya pili.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Masuala ya Taasisi ya Kampuni ya Lake Oil, Bw. Stephen Mtemi, amewasilisha taarifa kamili kwa ujumbe wa DART kuhusu hatua zilizofikiwa na mipango ya baadaye ya ujenzi wa miundombinu ya CNG.
“Tumesaini mkataba na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa muhimu. Baadhi ya vifaa hivyo vinatoka nje ya nchi, na endapo kutakuwa na ucheleweshaji wowote, tumejiandaa kutumia vitengo vya muda vya kujaza gesi,” amesema Bw. Mtemi.
Amefafanua kuwa endapo vifaa kutoka nje vitachelewa kufika, kampuni yao iko tayari kutumia vyombo vinavyoweza kutembezwa ili kuhakikisha kuwa mabasi yanaendelea kupata gesi bila kukwama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lake Oil, Bw. Biji Alappat, ameihakikishia Wakala wa DART kuwa kampuni yao inafanya kazi usiku na mchana kukamilisha miundombinu hiyo kwa wakati. “Tuna timu ya kiufundi tayari kusimamia usimikaji wa vifaa pindi vitakapowasili,” amesema.
Afisa mwingine mwandamizi wa Lake Oil, Bw. Dileep Kumar, amesema kuwa kazi za awali katika karakana ya Mbagala zimeanza, na wiki ijayo wataalika maafisa wa DART kutembelea eneo hilo kuona maendeleo hayo.
Dkt. Kihamia ameonesha kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Lake Oil na TPDC, na kupongeza ushirikiano mzuri uliopo. “Tunaridhika na juhudi zinazofanyika, hasa hatua za tahadhari na mipango ya muda mfupi iliyowekwa,” amesema.
Kuhusu usalama, Bw. Mtemi amefafanua kuwa kampuni yao inafuata viwango vya kimataifa na kanuni za kitaifa za usalama katika ushughulikiaji wa gesi ya CNG. “Tunaweka mifumo ya kuzima moto, teknolojia ya kugundua uvujaji wa gesi, na tunatoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu kwa kushirikiana na vyombo vya usalama,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa kampeni za uhamasishaji pia zitafanyika kwa madereva, wahudumu na mafundi kuhusu matumizi salama ya gesi hiyo pamoja na hatua za kuchukua endapo ajali itatokea.
Lake Oil imepanga kuweka vituo vya kujaza CNG katika maeneo mbalimbali ya Awamu ya Pili ili kuongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa magari kwenye karakana kuu.
Dkt. Kihamia amesisitiza kuwa Awamu ya Pili inaleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa DART kwa kutumia nishati safi, sambamba na ajenda ya kitaifa ya kupunguza hewa ya ukaa na kuboresha usafiri wa jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa DART umeupongeza Lake Oil kwa uwazi na ushirikiano wake, na kusema kuwa ziara hiyo imeongeza imani kuwa maandalizi yapo kwenye mstari sahihi.