Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Dr. Kihamia afafanua hasara, ujenzi wa miundombinu kwa waandishi wa habari
25 Jul, 2025
Dr. Kihamia afafanua hasara, ujenzi wa miundombinu kwa waandishi wa habari

Baada ya hotuba rasmi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, waandishi wa habari walielekeza maswali kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, Dkt. Athumani Kihamia, kuhusu hasara zilizopatikana na hali ya mikopo ya Benki ya Dunia katika ujenzi wa miundombinu ya BRT.

Akijibu swali kuhusu kiwango cha hasara iliyosababishwa na utoaji wa huduma duni kutoka kwa Mtoa Huduma wa Mpito (UDART), Dkt. Kihamia ameeleza kuwa lengo kuu la mradi wa BRT si kupata faida ya kifedha bali kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwawezesha kufika kwa wakati kwenye shughuli zao.

“Hasara haitazamiwi kama hasara ya kifedha kwa Wakala, bali ni kwa namna gani wananchi wananyimwa fursa za kiuchumi kwa kushindwa kufika kazini, sehemu za biashara au kwenye shughuli nyingine kwa wakati,” amesema Dkt. Kihamia.

Amesisitiza kuwa usafiri wa umma una mchango mkubwa katika kukuza uzalishaji na kuharakisha uchumi wa Jiji la Dar es Salaam. “Gari likichelewa au kuharibika mara kwa mara, uchumi hupungua kasi kwa sababu ya kupoteza muda wa kazi na biashara kuvurugika,” ameongeza kusema.

Dkt. Kihamia amesema kuwa Serikali inafahamu changamoto zilizopo na iko mbioni kuondoa huduma ya mpito. Alieleza kuwa Watoa Huduma wapya wa Awamu ya Kwanza na ya Pili wataleta jumla ya mabasi mapya 877 kuanzia Agosti na Oktoba mwaka huu.

Swali jingine muhimu limeulizwa na waandishi wa habari limehusu mikopo kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya BRT. Wametaka kufahamu iwapo mikopo hiyo imeleta mafanikio kwa mradi huo.

Akijibu, Dkt. Kihamia amesema kuwa mikopo hiyo imekuwa na mafanikio makubwa, akieleza hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa miundombinu. “Serikali imekamilisha kwa mafanikio Awamu ya Kwanza na ya Pili, na sasa Awamu ya Tatu na ya Nne ziko katika hatua nzuri,” amesisitiza.

ametaja urefu wa barabara kwa kila awamu: Awamu ya Kwanza ina kilomita 20.9 (barabara ya Morogoro), Awamu ya Pili kilomita 20.3 (barabara ya Kilwa), Awamu ya Tatu kilomita 23.6 (barabara ya Nyerere), na Awamu ya Nne ni kilomita 30.1 (barabara ya Bagamoyo kuelekea Tegeta).

“Maendeleo haya ya miundombinu yasingewezekana bila msaada madhubuti kutoka Benki ya Dunia na wadau wengine,” amesema Dkt. Kihamia.

Ameongeza kuwa Utaalam Ushauri wa Watoa Huduma kwa Awamu ya Tatu na ya Nne unaendelea kupitia usaidizi wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), kwa lengo la kuhakikisha huduma zinaanza mara moja miundombinu inapokamilika.

Dkt. Kihamia amewahakikishia wananchi kuwa huduma zitaboreshwa mara tu mabasi mapya yatakapoanza kazi rasmi chini ya Watoa Huduma wapya.

Amewashukuru waandishi wa habari kwa kuibua hoja zinazowakilisha sauti ya wananchi na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa uwazi na uwajibikaji.

Mkutano huo pia umeeleza mpango mpana wa Serikali wa kubadili mfumo wa usafiri jijini kuwa wa kisasa, safi na rafiki kwa mazingira kupitia teknolojia na ushirikiano wa PPP.

Mtendaji Mkuu wa DART amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kuwa na subira kwani hatua kubwa zimepigwa, na matokeo chanya yatadhihirika hivi karibuni.