Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
HOTUBA YA MHE. ANGELLAH KAIRUKI (MB), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, KATIKA UZINDUZI WA BODI YA USHAURI YA WIZARA YA WAKALA WA MABASI YAENDAYO HARAKA
19 Feb, 2023 Pakua

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa,

Prof. Riziki Shemdoe;

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka,

Dkt. Florence Martin Turuka;

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala-DART;

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART,

Dr. Edwin P. Mhede;

Timu ya Menejimenti ya Wakala;

Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kumkaribisha Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara katika uzinduzi wa Bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambayo inaundwa na nyie. Pamoja na uzinduzi wa Bodi yenu, hafla hii inatoa fursa kwa Wajumbe kufahamiana na kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kutekeleza wajibu na majukumu yenu.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Kama mnavyofahamu Serikali kupitia Tangazo la Serikali Namba 120 la tarehe 25 Mei 2007 iliamua kuanzisha Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam kwa lengo kutatua changamoto ya aidha ya usafiri iliyokuwepo katika Jiji hilo. Pamoja na uwepo wa watoa huduma wengine katika Jiji bado uwezo wao ulikuwa hauendani na ukuaji wa jiji hususan uongezekaji wa idadi ya watu na shughuli za maendeleo jijini hivyo, kuona umuhimu wa kuanzisha usafiri wa Umma.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Uanzishaji wa chombo hiki cha Serikali chini ya usimamizi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ni muhimu kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi.  Aidha, chombo hiki kina wajibu wa kuhakikisha kinasimamia utekelezaji na uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es salaam ili azma ya Serikali katika uanzishaji wake iweze kutumia.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka unalenga kuboresho usafiri wa umma kuanzia miundombinu na utoaji wa huduma ya usafiri wa umma kwa kutumia vyombo vya usafiri ambavyo vinarahisha wasafiri kufika sehemu za biashara na kurudi nyumbani baada ya muda wa kazi bila kupoteza muda mwingi njiani kwa sababu ya msongamano wa magari barabarani.

Kwa tafiti ambazo zimefanywa na wadau wa maendeleo hususan Benki ya Dunia kuhusu Miji inayokuwa kwa haraka kama ilivyo jiji la Dar es Salaam na majiji mingine duniani, zinaonyesha pamoja na ukuaji wake hayajaweza kufikia kiwango cha kuchangia uchumi wa nchi zao na kuweza kupunguza kiwango cha umaskini kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo sekta ya usafiri wa umma.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Ni dhahiri kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi katika miji mikubwa inaenda polepole kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu ambayo mara nyingi haiendani na kasi ya uboreshaji wa miundombinu katika miji, uhaba wa fedha wa kujenga miundombinu inayokidhi mahitaji ya watu pamoja na kutokuwa na usimamizi makini katika miji husika.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Ongezeko la idadi ya watu katika miji mikubwa kwa mwongo uliopita limekuwa kubwa zaidi kuliko kasi ya uboreshaji wa miundombinu na hivyo kwa kiwango kikubwa kuongeza msongamano wa magari barabarani hasa wakati wa asubuhi ambapo wengi wa wakazi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam huenda kwenye sehemu zao za kazi, na wakati wa jioni wakirudi kutoka sehemu zao za kazi.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuamua kutekeleza mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART kumekuwa na tija kubwa sana, matokeo ambayo yanaonekana sasa ni pamoja na kupuguza muda wa kusafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutoka masaa matatu hadi kufikia dakika 40 kwa Awamu ya Kwanza kutoka Kimara hadi Kivukoni. Hii imewezekana kutokana na usanifu wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka ambayo ina njia pekee kwa ajili ya mabasi yanayotumika katika mfumo huu mpya wa usafiri wa umma. Lakini pia mabasi haya ni makubwa na yenye uwezo wa kubeba abiria wengi kwa wakati mmoja.

 

Aidha, huduma ya mabasi inayotolewa katika Awamu ya Kwanza katika Barabara ya Morogoro na matawi yake si tu kubeba abiria wengi kwa pamoja mradi huu umeleta mageuzi kwa watumiaji wote wa barabara kwa kuwepo kwa njia pekee za mabasi, kuwepo kwa njia za waenda kwa miguu na njia za waendesha baiskeli.

 

Ndugu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa Bodi, Uzinduzi wa Bodi hii umekuja wakati muafaka ambapo hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametangaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti mwaka huu ambapo idadi ya watu katika Taifa letu imefika Milioni 61.7 huku Jiji la Dar es Salaam likiwa na wakazi Milioni 5.4. Hii inaashiria kuwa miji yetu inaendelea kukua kwa kasi hivyo mahitaji ya uboreshaji wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka ni jambo la lazima hususan katika kutekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ili kurahisha usafiri wa watu katika jiji la Dar es Salaam na miji mingine ya Tanzania ambayo itakuwa na sifa za kuanzisha mradi kama huu.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Kutokana na kazi zinazoendelea katika ujenzi wa miundombinu Awamu ya Pili kwa barabara iendayo Mbagala Rangitatu, na huduma ya mabasi inayoendelea Awamu ya Kwanza katika Barabara ya Morogoro na maeneo mengine kama vile Hospitali ya Mloganzila na Kibaha, ni dhahiri kuwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART, unatakiwa kujipanga kupambana na changamoto za usafiri wa umma zitakazoongezeka katika jiji la Dar es Salaam.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Ni Dhahiri kuwa ili kuwepo na maendeleo ya mfumo wa usafiri wa umma katika jiji lolote duniani kunahitajika uongozi imara wenye maono makubwa katika kutoa huduma ya usafiri wa umma iliyo bora. Kutokana na usimamizi imara unaofanywa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI katika kutekeleza mradi wa DART, jiji la Dar es Salaam limefanya uamuzi thabiti wa kutoa huduma hii ya usafiri katika ubora wa kiwango cha kimataifa.

 

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Bodi ya Ushauri inayozinduliwa leo ni sehemu ya uongozi ambao unategemewa kuwa na maono makubwa katika kuishauri Wizara kwa namna bora Wakala wa DART utasimamia mradi huu ili iweze kuleta tija katika kuwahudumia wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na nchi nzima.

Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan iko mstari wa mbele katika kuweka uongozi wenye kutoa kila aina ya msaada kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam ambalo linachangia kwa asilimia 80 katika pato la Taifa.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Rai yangu kwa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa DART ambayo tunaizindua leo ni kuitaka ihakikishe inafanya kazi kwa bidii katika kubuni mikakati ya kuboresha zaidi huduma ya usafiri ndani ya Jiji la        Dar es Salaam na ikiwezekana kuchukua hatua za kuanzisha huduma hii katika majiji mengine nchini ambayo yamekidhi vigezo vya kutekeleza mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka hasa kwa kuzingatia ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi  iliyobainisha ongezeko la watu katika kila Mkoa.

Ndugu Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi, Napenda kuwapongeza tena Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri kwa kuteuliwa kuwa katika Bodi hii. Ni imani yangu kuwa mtafanya kazi yenu kwa weledi wa hali ya juu katika kuishauri Wizara juu ya namna bora Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka utakavyosimamiwa ili iwe na mipango yenye kuleta tija kwa kuongeza mapato ya Wakala na kuondokana na utegemezi kutoka Serikalini.  Aidha Bodi katika ushauri wenu hakikisheni mnazingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa mradi huu muhimu.

Baada ya kusema hayo, ninachukua nafasi hii kutamka kuwa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imezinduliwa rasmi.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA