Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Dk.Mhede ataka watumishi DART kufanya kazi kwa bidi ili kuboresha utoaji wa huduma
21 Apr, 2023
Dk.Mhede ataka watumishi DART kufanya kazi kwa bidi ili kuboresha utoaji wa huduma

Wakati mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ukiendelea kujenga miundombinu yake na kuongeza huduma katika barabara ya Kilwa kuelekea Mbagala na katika Barabara ya Nyerere kuelekea Gongolamboto, watumishi wa Wakala huo wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma na kuongeza ubunifu zaidi ili kuwapa huduma bora ya usafiri wa umma wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa DART Dr.Edwin.P.Mhede katika mkutano wa 9 wa wafanyakazi wa DART ambapo alisisitiza kuwa utendaji kazi uliotukuka ndio kigezo cha kufanya Wakala uonekane unatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumzia tabia za kutowajibika na kutofuata sheria na kanuni za utumishi wa umma Mtendaji Mkuu alikemea tabia ya uchelewaji kwa baadhi ya watumishi jambo ambalo linarudisha nyuma utoaji huduma bora kwa wananchi.

Sambamba na hilo Dkt. Mhede pia aliwataka watumishi kushiriki kushiriki bila kukosa katika matukio mbali mbali ya Wakala huo yakiwemo yale ya Michezo na Mabonanza  kwani ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kwamba kwa watumishi wa umma kila tukio rasmi ni sehemu yao ya kazi hivyo hawatakiwi kukosa.

Mbali na kufanya kazi kwa bidii, aliwakumbusha watumishi hao kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2019 kifungu cha 298, Pamoja na kanuni za utumishi wa umma Namba 444 za mwaka 2022 zinazoelekeza namna bora ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kiutumishi.

Dr.Mhede alifafanua kuwa, watumishi wa umma pia wanaongozwa na maadili ya utendaji kazi katika kuhudumia wananchi, hivyo wanapaswa kuzingatia utii kwa Serikali,kuheshimu sheria,uadilifu, usawa,uwajibikaji, ubunifu na kujitahidi kutunza siri na taarifa rasmi za Serikali.

Aidha aliwata wasimamizi wa kazi na wakuu wa Idara na vitengo kuwaheshimu walioko chini yao na kuwatendea haki bila ubaguzi wa aina yoyote, pia aliwataka watumishi kuheshimu ngazi za utendaji mahala pa kazi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

“Tunaongozwa na falsafa ya kuweka mioyo yetu katika kazi na sio kuweka kazi katika mioyo yetu ili tuweze kupata matokeo chanya,Pamoja na kuwa waaminifu, kepuka uvivu, rushwa Pamoja na tabia zote zisizofaa kwa watumishi wa umma lakini pia kwa jamii ya watu waliostaarabika”Alisema.

Dr.Mhede pia alitumia fursa hiyo pia kumshukuru Mh. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha muundo mpya wa Wakala jambo ambalo limeongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa DART.

Kwa upande wao baadhi ya watumishi waliochangia katika kuboresha utendaji kazi wa Wakala akiwemo  Bw. Geofrey Mgegwa, kutoka kitengo cha Uhasibu alisema kuwa wosia wa Mtendaji Mkuu ni fursa nzuri kwake na Wakala kwa ujumla kwani umewakumbusha watumishi kufanya kazi kwa bidii na kujituma jambo ambalo ndilo nguzo kubwa ya mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake mmoja wa madereva wa Wakala huo Bw.Zebu Mtawa, alisema ni jambo la busara kwa Mtendaji Mkuu kukaa na kuwakumbusha watumishi mambo muhimu ya kuzingatia katika utendaji kazi hivyo kufanya huduma kuendelea kuwa bora Zaidi, ikizingatiwa kuwa utoaji huduma ya usafiri wa umma una changamoto nyingi.

“Binafsi nimeyapokea maelekezo ya Mtendaji Mkuu lakini pia niwakumbushe wenzangu kuwa mafanikio yoyote yanakuja kwa kufanya kazi kwa bidii hivyo hakuna kazi nyingine iliyobaki Zaidi ya kufanya kazi Zaidi ili hata Imani ya Mkuu wa Nchi kwa Wakala iongezeke” Alisema Bw.Mtawa.

Kwa upande wake Bw. Bwana Malima, ambaye ni Afisa Biashara Mkuu wa DART, alisema kuwa ni vyema kuzipenda na kuzithamini kazi zetu za kila siku na kuongeza ubunifu Zaidi bila kujali wakati au mahali ambapo mtumishi atakuwepo.

Naye Bwana Robert Kagali,ambaye ni Afisa wa Utawala wa Wakala, alisema kuwa ikiwa kila mtumishi atatekeleza majukumu yake kama alivyoelekezwa na Mtendaji Mkuu ana uhakika changamoto nyingi zinazoukabili wakala zitakwisha kabisa.

Afisa Habari Mwandamizi wa Wakala huo Bi.Martha Komba, alisisitiza watumishi kuacha uvivu badala yake kufanya kazi kwa bidi na kuongeza ubunifu ili kufikia malengo ya Wakala ya kutoa usafiri wa umma nadhifu katika mkoa wa Dar es Salaam.

Katika mkutano huo wa 9 wa watumishi wote wa Wakala, mada mbalimbali zilitolewa na Maafisa kutoka taasisi zilizoalikwa wakiwemo Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU ambao waliotoa mada juu ya umuhimu wa watumishi kuepuka kujihusisha katika vitendo vya rushwa.

Pia kulikuwa na mtoa mada kutoka Manispaa ya Ubungo ambaye aliwaongoza watumishi kujadili uanzishwaji wa ushirika wa kuweka na kukopa SACCOS ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka.

Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Mkoa wa Dar es Salaam umepangwa kutekelezwa katika awamu sita, ukihusisha mtandao wan jia maalum kwa ajili ya Mabasi pekeyake wenye urefu wa kilometa  154.4 , aidha kutokana na ukuaji wa miji na maendeleo ya kiuchumi na kibiashara mtandao huo unaweza kuongezeka Zaidi kulingana na mahitaji ya baadaye.

Ujenzi wa miundombinu ya BRT kwa Awamu ya kwanza yenye kilomita 20.9, ulikamilika mwaka 2015, ambapo utoaji wa huduma ya Mabasi ulianza 10 Mei 2016, chini yam toa huduma wa kipindi cha mpito.

Maendeleo ya miundombinu ya BRT kwa Awamu ya pili katika barabara ya Kilwa  ambayo imefikia 90% inakadiriwa kukamilika mwishoni mwa 2023. Maendeleo ya miundombinu ya BRT kwa Awamu ya tatu ambayo iko katika hatua ya ujenzi itakamilika mwishoni mwa 2024, ambayo mara itakapokamilika huduma ya Mabasi itaanzaikifuatiwa na operesheni ya mabasi mwaka 2025.