Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART Yapongezwa Matumizi ya TEHAMA, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI aelekeza Taasisi nyingine kuiga mfano.
27 Jul, 2023
DART Yapongezwa Matumizi ya TEHAMA, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI aelekeza Taasisi nyingine kuiga mfano.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi; ya Rais TAMISEMI; anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ameupongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)  kwa namna unavyotumia mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya Serikali.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Julai 26, 2023 wakati wa ziara yake katika Wakala wa DART, Mhandisi Mativila alisema matumizi ya TEHAMA ni mwarobaini wa uvujaji wa mapato ya serikali hivyo ni vyema kila taasisi ikajikita katika kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji na udhibiti wa mapato.

“ Mifumo ikitumika vizuri kwanza inarahisisha utendaji wa kazi na inaleta ufanisi lakini pia inaondoa kabisa matatizo ya uvujaji wa mapato, hivyo naelekeza taasisi nyingine zilizoko chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuiga hatua hizi njema ambazo wenzetu wa DART wanazichukua na kuzitekeleza” Alisema.

Aidha Mhandisi Mativila alisema mradi wa maendelezo yatokanayo na maboresho ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (TOD) unaohusisha kuendeleza maeneo ya pembezoni mwa ushoroba wa mradi wa DART, utausaidia Wakala kupata vyanzo vya mapato nje ya kutegemea nauli jambo ambalo litawapunguzia watumiaji wa Mabasi gharama za kupanda kwa nauli mara kwa mara.

Katika mradi wa TOD maeneo ya pembezoni mwa ushoroba wa DART kutakuwa na maduka makubwa ya kisasa, maeneo ya makazi, vivutio mbali mbali yakiwemo mahoteli Pamoja na sehemu za burudani jambo ambalo litayafanya maeneo hayo kuwa na thamani kubwa.

Akizungumza katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Edwin Mhede alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa Wakala umejipanga kuimarisha mifumo mbali mbali ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa kila siku.

“Kwa sasa tumeshakamilisha manunuzi ya Kadi janja na ziko tayari, tunasubiri tu mageti ya kuingilia vituoni yaje ili tufungamanishe mfumo na kuanza kutoa huduma ya kadi kwa wananchi wetu, hii itaondoa kabisa adha ya matumizi ya tiketi za karatasi ambazo sio rafiki kwa mazingira” Alisema.

 

Dkt. Mhede pia alimweleza Naibu Katibu Mkuu kuwa Wakala umejipanga kuhakikisha hadi ifikapo mwezi Machi,2024 huduma za usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Awamu ya Pili kuanzia Gerezani Kariakoo hadi Mbagala Rangitatu itakuwa imeanza hivyo wana Dar es Salaam na maeneo ya Jirani wakae mkao wa kuanza kutumia huduma.