Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Mkataba Ujenzi wa Mindombinu ya Mradi wa DART Awamu ya Nne Kuelekea Tegeta Wasainiwa.
24 Jul, 2023
Mkataba Ujenzi wa Mindombinu ya Mradi wa DART Awamu ya Nne Kuelekea Tegeta Wasainiwa.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa DART,  Juni 30, 2023 imesaini mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya Mradi huo kwa Awamu ya Nne inayoelekea Tegeta.

Mkataba huo umesainiwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta kwa niaba ya Serikali na Kampuni ya Shandong Luqiao Group pamoja na Kampuni ya China Communication Construction zote kutoka nchini China.

Zoezi la utiaji saini limeshuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi  Mheshimiwa Geofrey Kasekenya (Mb) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius  Nyerere Dar es Salaam.

Ujenzi wa Awamu hiyo unataraji kutekelezwa katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza  ya mkataba huo wenye thamani ya Tsh. Bilioni 174.3 unatarajia kukamilika ndani miezi 18 ukihusisha barabara za Mabasi Yaendayo Haraka yenye urefu wa Kilomita 13.5 inayoanzia Maktaba Kuu ya Taifa hadi Mwenge, na kipande cha Barabara ya Sam Nujomakuanzia Mwenge hadi Ubungo.

Aidha ujenzi huo utakaotekelezwa na kampuni ya China Geo- Engineering Corporation utahusisha pia  upanuzi wa daraja la Selander, ujenzi wa Karakana, vituo vikuu vya mabasi viwili, vituo vidogo 20 pamoja na vituo mlishi 10.

Katika sehemu ya pili ya ujenzi huo kutoka Mwenge hadi Tegeta, utatekelezwa na Mkandarasi Shadong Luqiao Group ukihusisha upanuzi wa madaraja matatu ya Mlalakuwa, Kawe na Tegeta, ujenzi wa vituo 19 vya mabasi pamoja na vituo mlishi vitano.

Vilevile ujenzi wa miundombinu hiyo  kwa sehemu ya pili unaohusisha barabara yenye urefu wa Kilomita 15.6, unataraji kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 na unatekelezwa kwa gharama ya Tsh. Bilioni 193.8.

Ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka katika Mkoa wa Dar es Salaam imepangwa kutekelezwa katika awamu sita ambapo Awamu ya Kwanza kuanzia Kimara hadi Kivukoni na matawi yake ya Magomeni hadi Moroco na Fire hadi Gerezani Kariakoo, ujenzi wake umekamilika na huduma kutolewa huku Awamu ya Pili kuelekea Mbagala na Awamu ya Tatu Kuelekea Gongolamboto ujenzi wake ukiendelea.

Aidha, Awamu ya Tano itahusisha Barabara ya Mandela kutokea Ubungo hadi Daraja la Mwalimu Nyerere kuelekea Kigamboni, na matawi yake kuanzia Kigogo makutano kupitia Tabata Dampo hadi Segerea, wakati Awamu ya Sita itahusisha Barabara za Mwai Kibaki Morocco hadi Kawe na nyongeza ya Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka kuanzia Kimara hadi Kibaha, Pamoja na barabara kutoka Mbagala Rangitatu hadi Vikindu.

Ujenzi wa miundombinu hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupunguza kero ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.