LATRA yahamishia huduma za daladala Kituo Kikuu BRT Mbagala
Serikali imetangaza mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za usafiri wa umma katika ukanda wa Mbagala kwa kuzielekeza daladala zote zinazotumia kituo kidogo cha Mbagala Rangi Tatu na maeneo ya kando ya barabara kuhamia rasmi ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Mbagala kuanzia Julai 1, 2026.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia ziara ya pamoja ya kikazi iliyofanywa Juni 15, 2026 na viongozi wa juu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam-DART, pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini-LATRA, waliokagua maendeleo ya miundombinu na mifumo ya utoaji huduma katika eneo hilo.
Mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kubadilisha mfumo wa usafiri wa umma kutoka utegemezi mkubwa wa daladala kwenda mfumo wa usafiri wa watu wengi unaotumia mabasi ya mwendokasi katika njia maalumu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Said Habibu Tunda, aliridhia rasmi matumizi ya kituo mlishi kilichopo ndani ya Kituo Kikuu cha BRT Mbagala kwa ajili ya daladala kupakia na kushusha abiria.
Bw. Tunda alisema kuwa kuanzia Julai 1, 2026 kituo hicho kitaanza kutumika na daladala zinazotoka Kongowe, Vikindu, Tuangoma, Mkuranga na maeneo mengine ya jirani.
“Tumekubali eneo hili la kituo mlishi litumiwe na wenzetu wa daladala kuanzia Julai 1, 2026 ili kurahisisha muunganiko wa usafiri kwa abiria wetu,” alisema Bw. Tunda.
Alifafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa usumbufu wa wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta usafiri wa kuunganisha safari zao pamoja na kupunguza msongamano wa magari nje ya kituo hicho.
Bw. Tunda aliwahakikishia madereva, makondakta na wamiliki wa daladala kuwa hakuna atakayepoteza ajira kutokana na mabadiliko hayo.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za usafiri na kwamba lengo la mpango huo si kuwaondoa katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa mujibu wake, dhamira kuu ni kuziunganisha daladala katika mfumo rasmi wa usafiri wa kisasa wenye tija zaidi kwa waendeshaji na wananchi wanaotumia huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habibu Suluo, alisema daladala zote zinazotumia kituo kidogo cha Mbagala Rangi Tatu pamoja na vituo visivyo rasmi kandokando ya barabara zinapaswa kuhamia katika kituo kipya ifikapo Julai 1, 2026.
Dkt. Suluo alieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha udhibiti wa huduma za usafiri, usimamizi wa mtandao wa usafiri wa umma na kuongeza usalama wa abiria.
Aliongeza kuwa kuhamishia huduma zote katika kituo kilichopangwa kutapunguza msongamano wa magari, kuboresha mtiririko wa usafiri na kuongeza ufanisi wa mfumo wa BRT Awamu ya Pili.
DART na LATRA zimesisitiza kuwa zitaendelea kushirikiana na waendeshaji wa usafiri pamoja na wananchi ili kuhakikisha utekelezaji wa mabadiliko hayo unafanyika kwa mafanikio na hatimaye kuimarisha huduma za usafiri wa umma jijini Dar es Salaam
