Mradi wa DART Awamu ya Tatu
Mradi wa DART Awamu ya Tatu
Awamu ya Tatu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ni mojawapo ya miradi muhimu ya upanuzi wa mfumo wa usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam. Awamu hii inalenga kuunganisha jijni kati, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), maeneo ya viwanda na makazi yanayokua kwa kasi. Awamu ya Tatu ina jumla ya urefu wa kilomita 23.6. Ushoroba mkuu unaanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mitaa ya Azikiwe na Maktaba, ukipitia Barabara za Bibi Titi na Nyerere hadi Gongo la Mboto. Tawi lingine linaanzia Kituo Kikuu cha Gerezani kupitia Mtaa wa Lindi, Shaurimoyo, Barabara ya Uhuru na Buguruni kabla ya kuungana na Barabara ya Nelson Mandela na baadaye kuingia kwenye Barabara ya Nyerere eneo la TAZARA. Awamu ya Tatu imeundwa kuunganishwa na awamu nyingine za DART kupitia vituo muhimu vya Gerezani na Kivukoni, hivyo kuongeza ufanisi wa mtandao mzima wa usafiri wa umma. Mradi unahusisha ujenzi wa njia maalum za mabasi, barabara za magari mengine, njia za watembea kwa miguu, njia za baiskeli, mifereji ya maji ya mvua, makutano ya barabara na miundombinu mingine ya usafiri. Sehemu muhimu ya mradi ni ujenzi wa vituo vya kisasa vya abiria vinavyowezesha kupanda na kushuka kwa usalama, pamoja na mifumo ya taarifa kwa abiria na huduma za watu wenye mahitaji maalum. Mradi unajumuisha vituo vikuu vitatu vya mabasi pamoja na vituo mlishi vitatu vitakavyorahisisha uhamaji wa abiria kati ya njia kuu na huduma za mlishi. Awamu hii pia inahusisha ujenzi wa karakana ya kisasa pamoja na karakana ndogo za matengenezo zitakazotumika kwa maegesho, matengenezo na usimamizi wa mabasi. Fungu la kwanza la ujenzi kilianza mwezi Agosti 2022 na kwa sasa kimefikia hatua za mwisho za utekelezaji. Taarifa za maendeleo zinaonesha kuwa kazi za miundombinu ya barabara zimefikia takribani asilimia 99 ya utekelezaji. Fungu la pili la ujenzi lilianza mwezi Novemba 2025 na linahusisha miundombinu ya uendeshaji pamoja na sehemu za karakana. Mkandarasi anaendelea na kazi za awali ikiwemo usafishaji wa eneo, maandalizi ya eneo la mradi na ujenzi wa ofisi za muda. Fungu la kazi ya ujenzi wa miundombinu linatarajiwa kukamilika mwaka 2026, huku fungu la pili linalojumuisha karakana na miundombinu inayohusiana nalo linatarajiwa kukamilika mwaka 2027. Baada ya kukamilika, Awamu ya Tatu itarahisisha usafiri kati ya katikati ya jiji, uwanja wa ndege, maeneo ya viwanda na makazi. Mradi utapunguza muda wa safari, kuongeza usalama barabarani na kuchangia maendeleo ya uchumi na usafiri endelevu nchini Tanzania.
