MFUMO WA DART AWAMU YA KWANZA
MFUMO WA DART AWAMU YA KWANZA
Awamu ya Kwanza ya Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ndiyo ushoroba wa kwanza wa DART uliojengwa katika Jiji la Dar es Salaam. Awamu hii imeweka msingi wa mfumo wa kisasa wa usafiri wa umma wenye uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi kwa ufanisi na kupunguza msongamano wa magari. Awamu ya Kwanza ina urefu wa kilomita 20.9 na inajumuisha Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni (km 15.7), Barabara ya Kawawa kutoka Morocco hadi Magomeni (km 3.6), na Barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Kariakoo/Gerezani (km 1.6). Ushoroba huu unaunganisha maeneo muhimu ya makazi, biashara na huduma za kijamii na hivyo kurahisisha usafiri kati ya vitongoji vya jiji na kitovu cha biashara cha Dar es Salaam. Ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ulianza mwaka 2012 na kukamilika kwa kiasi kikubwa mwaka 2015, kabla ya huduma rasmi za mabasi kuanza mwezi Mei 2016. Miundombinu ya Awamu ya Kwanza inajumuisha njia maalum za mabasi zilizotenganishwa na magari mengine, hatua inayosaidia kuongeza kasi, usalama na uhakika wa huduma. Mradi ulijumuisha ujenzi wa vituo vya kisasa vya abiria ambavyo vimewekwa katikati ya barabara pamoja na miundombinu ya tiketi, taarifa za usafiri na huduma za usalama. Vituo vikuu vya Kivukoni, Kimara, Ubugo, Morocco, na Gerezani vimejengwa kama sehemu muhimu ya mtandao wa usafiri na vinaendelea kuhudumia maelfu ya abiria kila siku. Awamu ya Kwanza ilijumuisha miundombinu ya karakana kwa ajili ya maegesho, matengenezo ya mabasi na usimamizi wa shughuli za uendeshaji wa mfumo. Kuna karakana ndogo iliyopo Ubungo, na karakana nyingine ambazo ziko katika hatua ya kujengwa katika awamu hii. Mradi unahusisha uboreshaji wa barabara, makutano, mifumo ya usimamizi wa trafiki na maeneo ya kuvuka barabara kwa lengo la kuongeza usalama na ufanisi. Njia za watembea kwa miguu, madaraja ya kuvukia na miundombinu ya kuwezesha watu wenye mahitaji maalum zimejengwa ili kuboresha usalama na upatikanaji wa huduma. Katika miaka ya karibuni, Awamu ya Kwanza imeboreshwa kwa kuingizwa kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Nauli (AFCS), mageti janja na teknolojia nyingine za usimamizi wa huduma. Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya Awamu ya Kwanza kupitia miradi ya ukarabati na upanuzi wa baadhi ya sehemu za barabara pamoja na miundombinu inayounganisha ushoroba huu. Awamu ya Kwanza imechangia kupunguza muda wa safari, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, na kuongeza tija kwa wakazi wa Dar es Salaam. Kama msingi wa mtandao mzima wa DART, Awamu ya Kwanza inaendelea kuwa kiungo muhimu cha kuunganisha awamu nyingine za mradi na kufanikisha maono ya usafiri wa umma wa kisasa.
