News

​Austria yaonyesha nia kuwekeza katika Mabasi Yaendayo Haraka


Na. Mwandishi Wetu

Kampuni ya Utengenezaji Mabasi yanayotumia nishati jadidifu ya gesi ya ETEFA kutoka nchini Austria, imeonyesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kwenye eneo la Mabasi ya kisasa yanayotumia gesi badala ya mafuta.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika kikao baina ya kampuni ya ETEFA na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART, Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Johann Rieger amesema Kampuni yake ina uzoefu wa kutosha wa kutengeneza Mabasi ambayo hayatumii mafuta jambo ambalo ni rafiki wa mazingiza na pia linasaidia kupunguza gharama za uendeshaji.

“Mabasi tunayotengeneza yanatumia gesi na nimeelezwa kuwa Tanzania mnayo gesi ya kutosha hivyo ni fursa kwenu kutumia rasilimali hiyo kwa ajili ya kuendeshea Mabasi Yaendayo Haraka kwani kutumia gesi kuna punguza gharama za uendeshaji kutokana na matumizi ya mafuta kuwa ghali” Alisema Bw. Rieger.

Alisema endapo watapata fursa ya kuwekeza nchini Tanzania katika Mabasi Yaendayo Haraka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART itakuwa mdau wa kwanza nchini kutumia huduma hiyo na itakua fursa kwa nchi nyingine kuja kujifunza.

Mtendaji Mkuu huyo wa ETEFA alisema Tanzania kijiografia imekaa eneo zuri sana katika nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo ikianzisha kitu chochote ni rahisi kuenea kwa urahisi na kwa haraka katika nchi nyingine zinazoizunguka, hivyo kama ikianza kutumia gesi asilia kwenye Mabasi itapata faida kubwa kwani watauza gesi na ajira zitaongezeka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na maendeleo ya Biashara wa DART Bi. Susan Chaula amesema wamepokea wazo la wawekezaji hao na watalifanyia kazi kwani kwa sasa Tanzania ina rasilimali ya kutosha ya gesi asilia ambayo ikitumika katika Mabasi Yaendayo Haraka itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kutunza mazingira.

“Tumewapokea na tumewasikiliza kimsingi wana teknolojia ya kisasa kabisa kama walivyotuonyesha na kama wakifanikiwa kuwekeza hapa nchini sio tu tutapata faida ya kutumia gesi asilia tuliyo nayo, bali tutakua mfano duniani kwa kutumia nishati mbadala ambayo ni rafiki wa mazingira kama dunia inavyojielekeza kwa sasa” Alisema.

Mkurugenzi huyo aliwataka wawekezaji wengine watakaoona fursa za kuwekeza hapa nchini wasisite kuja kwani hata Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekua akisisitiza mara kwa mara kuwa wawekezaji wakaribishwe na wapewe ushirikiano wa kutosha kwani nchi yetu ni mahali salama pa kuwekeza.

Mwisho.
Tanzania Census 2022