Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Mtendaji Mkuu aagiza watumishi kuheshimu ushirikianao na uadilifu kazini
11 Dec, 2025
Mtendaji Mkuu aagiza watumishi kuheshimu ushirikianao na uadilifu kazini

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Said Tunda, amewataka watumishi wa Wakala huo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, uadilifu na weledi ili kuongeza ufanisi katika kuendeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT)  Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao chake cha kwanza na watumishi tangu kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bw. Tunda alisema ushirikiano wa dhati miongoni mwa watumishi ndiyo nguzo ya kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa umma kupitia mradi wa BRT unaotekelezwa kwa awamu sita chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Bw. Tunda alibainisha kuwa kila mtumishi ana jukumu muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi na hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa kujituma, kuwajibika na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu ya kazi na kuimarisha umoja ili kuhakikisha DART inaendelea kutoa huduma zinazoendana na matarajio ya wananchi na malengo ya Serikali katika kuboresha usafiri wa mijini.

Katika hotuba yake, Bw. Tunda alikiagiza Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kuandaa makala zitakazoeleza historia ya mradi, malengo yake, hatua ulipofikia na matarajio ya baadaye, ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mradi huo muhimu.

Kikao hicho pia kiliwapa fursa watumishi kutoa maoni, kueleza changamoto na kupendekeza maboresho yatakayosaidia kuinua utendaji. Bw. Tunda aliwahakikishia kuwa maoni yao yatapitiwa na kufanyiwa kazi ili kuongeza tija ya taasisi.

Aliongeza kuwa uongozi wake utaendelea kusimamia utamaduni wa kusikiliza watumishi na kushirikiana nao katika kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya taasisi.

Katika kikao hicho, Bw. Tunda alimpa nafasi Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Utafiti, Bw. Abdulrahman Mshiri, kuwaaga watumishi wenzake kutokana na kuhitajiwa kustaafu hivi karibuni.

Bw. Mshiri aliishukuru Menejimenti na watumishi wote kwa ushirikiano waliompatia na kuwasihi kuendeleza nidhamu na kujituma ili kufanikiwa katika utumishi wa umma.

Aidha, kikao kilijadili masuala ya ustawi wa kijamii ikijumuisha taarifa kuhusu Mfuko wa kusaidiana kwa watumishi maarufu kwa jina la DART Social Fund pamoja na chama cha ushirika cha akiba na mikopo – DART SACCOS.

Kikao kilimalizika kwa watumishi kuahidi kuongeza ushirikiano na kujituma zaidi katika kutekeleza majukumu ya kuendeleza mradi huo muhimu kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya nchi.