Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART KUENDELEA KUIMARISHA WATAALAM WAKE KUELEKEA MATUMIZI YA KADI JANJA
17 May, 2024
DART KUENDELEA KUIMARISHA WATAALAM WAKE KUELEKEA MATUMIZI YA KADI JANJA

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka – DART unaendelea kuimarisha wataalam wake wa Idara ya TEHAMA kuelekea matumizi ya kadi janja katika kulipia nauli kwenye huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka.

 

Hii imedhihirishwa leo Mei 17, 2024 baada ya wataalam hao kuhitimu mafunzo ya siku 5 ya M3-MIFARE DESIFIRE EV3/M4-MIFARE SAM AV2 ambayo yamewaongezea ujuzi zaidi katika kusimamia Mfumo wa Ukusanyaji Nauli AFCS.

 

Akifunga mafunzo hayo yaliyokwenda sambamba na utoaji wa vyeti kwa wahitimu, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka – DART, Dkt. Athumani Kihamia amewapongeza na kuwataka kuyafanyia kazi yale yote walivyojifunza.

 

“Lengo la DART ni kuwa na timu mbalimbali za vijana tutakaokaa nao kwa muda mrefu zaidi wakifanya kazi kwa ufanisi na kuifanya taasisi yetu iwe mahiri zaidi kwenye kila idara na kuongeza tija kwenye mradi” alisema Dkt. Kihamia.

 

Aidha, Dkt. Kihamia amesema kuwa kazi ya usimikaji wa mageti janja inaendelea na mpaka kufikia mwezi Juni 2024 anatarajia watumiaji wa huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka watakuwa wameanza kutumia kadi janja.

 

“Nichukue fursa hii kuwaomba Watanzania na wana Dar es Salaam waamini kuwa siku chache zijazo baada ya Mwezi wa sita tutaanza kutumia mageti yetu, mageti haya yatatumika katika mfumo wa nauli ili kuepusha uvujaji wa mapato, kuokoa muda kwa wasafiri kuwahi kufika kule wanakotaka kwenda ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira kwa kuacha matumizi ya tiketi za makaratasi” amesema Kihamia

 

Vilevile Dkt. Kihamia aliwaarifu Watanzania kuwa Wakala unaendelea na taratibu za kuongeza mabasi mengine ili kuondoa changamoto ya uchache wa mabasi iliyopo hivi sasa.

 

Dkt. Kihamia pia alikemea tabia ya uvamizi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo haraka hususani barabara kuacha mara moja kutumia njia hizo kwani mbali na kuhatarisha usalama wa abiria pia wanavuruga mzunguko wa mabasi na hivyo kuchelewesha huduma hiyo ya usafiri wa haraka kwa abiria.

 

Kufanyika kwa mafunzo kama haya ni juhudi za Serikali ya kuwaongezea ujuzi na uzoefu wa mifumo mbalimbali Wataalam wa ndani itakayoleta tija kwa Taifa kwani itakumbukwa Mfumo wa Ukusanyaji Nauli wa AFCS ulitengenezwa na Wataalam hao.