Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART yaweka historia: mabasi 99 yapelekwa Kituo Kikuu cha Mbagala kwa kuanza huduma ya mabasi awamu ya pili
30 Aug, 2025
DART yaweka historia: mabasi 99 yapelekwa Kituo Kikuu cha Mbagala kwa kuanza huduma ya mabasi awamu ya pili

Katika kile kilichoelezwa kuwa ni mapambazuko mapya ya usafiri wa umma kwa wakazi wa Dar es Salaam, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umefanikiwa kuhamisha mabasi 99 ya njia kuu kutoka bandarini hadi Karakana ya Mbagala usiku wa Agosti 29, 2025, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea uzinduzi wa Awamu ya Pili ya mfumo wa BRT katika Barabara ya Kilwa.

Mabasi hayo ya kisasa yaliyomilikiwa na Kampuni ya Mofat Company Limited, yalikamilisha taratibu za ushuru kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwasili Mbagala salama katika zoezi lililosimamiwa kwa karibu na Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athumani Kihamia, akishirikiana na timu ya menejimenti na vyombo vya usalama.

“Uhamishaji huu wa mabasi ni ishara ya mabadiliko halisi kwa wakazi wa Mbagala na Jiji lote la Dar es Salaam,” alisema Dkt. Kihamia. “Sasa ni dhahiri kuwa serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kuboresha usafiri wa umma.”

Kwa mujibu wa Dkt. Kihamia, tukio hilo si tu kuwasili kwa mabasi bali ni ujumbe kwa watumiaji wa BRT na Watanzania kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kasi na umakini mkubwa.

“Hii ni matokeo ya usimamizi thabiti. Tangu mwaka 2024, tumefanikisha kusaini mikataba na watoa huduma kwa muda mfupi sana,” aliongeza, akibainisha kuwa viongozi wengi wa serikali wakiwemo makatibu wakuu wamepongeza kasi ya utekelezaji ya DART.

Kampuni ya Mofat, ambayo imepewa dhamana ya kutoa huduma za njia kuu kwa Awamu ya Pili, inatarajiwa kuwasilisha mabasi 255 mwaka huu. Tayari kampuni hiyo imeshaleta mabasi 99, na mabasi mengine 52 yamewasili bandarini yakisubiri kibali.
Muhammad Abdullah Kassim, Mtendaji Mkuu wa Mofat, alisema mabasi hayo yamejengwa kwa viwango vya kimataifa na yamefungwa viyoyozi (AC) na kamera za CCTV. “Tunataka kutoa huduma bora Afrika na kuwa kampuni bora ya usafiri barani,” alisema.

Mabasi hayo yakiwa Mbagala, kilichosalia kabla ya huduma kuanza ni kukamilika kwa miundombinu ya kujaza gesi (CNG) na usimikaji wa geti janja za kukata tiketi (AFCS).

Dkt. Kihamia aliwataka wakazi wa Mbagala na watumiaji wote wa BRT kuitunza miundombinu, kuepuka matumizi mabaya, na kuhakikisha usalama katika vituo vyote.

Mbali na Mofat, waendeshaji wengine wa njia za mlisho kwa Awamu ya Pili ni Metro City Link watakaotoa huduma katika njia 13 kwa kutumia mabasi 334, na YK City Link watakaoendesha njia 6 kwa kutumia mabasi 116.

Awamu ya Pili ikianza kikamilifu, itaboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wa usafiri wa umma na kupunguza msongamano wa magari kwenye Barabara ya Kilwa, hasa kwa wakazi wa maeneo ya kusini mwa Dar es Salaam.
Mradi wa BRT unatekelezwa kwa awamu sita, ambapo Awamu ya Kwanza (Barabara ya Morogoro) tayari imekamilika, na Awamu ya Pili iko hatua ya mwisho kabla ya uzinduzi rasmi wa huduma ya mabasi.

Uhamishaji wa mabasi umefungua ukurasa mpya kuelekea uzinduzi rasmi wa huduma za BRT kwa Awamu ya Pili, unaotarajiwa kufanyika wiki chache zijazo.