DART na AzamPay kufungamanisha kadi za kielektroniki kwa usafiri wa BRT

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) leo imekutana na kampuni ya AzamPay, tawi la Bakhresa Group, kwa ajili ya kujadili njia za kufungamanisha kadi ya Mwendokasi ya DART na kadi ya Azam kwa ajili ya malipo ya usafiri katika mfumo wa BRT katika awamu zote.
Kikao hicho kilifanyika katika ofisi za DART na kuwakutanisha wataalamu wa TEHAMA kutoka pande zote mbili. Uongozi wa DART uliongozwa na Mkurugenzi wa TEHAMA, Dkt. Zanifa Omary, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, akiwa na maafisa waandamizi wa Idara yake.
Kwa upande wa AzamPay, waliongozwa na Bw. Ibrahim Awadhi Shoo, Meneja wa Maendeleo ya Biashara, ambaye alieleza nia ya kampuni yao kupanua huduma za kidijitali kupitia mfumo mkubwa wa usafiri wa umma nchini.
Mpango huo unalenga kuruhusu abiria wa BRT kutumia kadi ya Azam kulipia nauli, sambamba na kadi ya Mwendokasi, kupitia mfumo wa ‘Automated Fare Collection System (AFCS)’ wa DART.
Majadiliano yalijikita kwenye mfungamanisho wa kimfumo, urahisi kwa watumiaji, na jinsi miundombinu ya pamoja itakavyofanya kazi kwa ufanisi kwenye vituo na ndani ya mabasi.
Kwa upande mwingine, AzamPay itafaidika kwa utangazaji mkubwa wa chapa yao kibiashara (brand visibility) kupitia mfumo wa BRT, kwa kuwa maelfu ya abiria watakuwa wakitumia kadi hiyo kila siku.
Dkt. Zanifa Omary alisifu mpango huo na kusisitiza kuwa makubaliano yoyote lazima yawe kwa manufaa ya abiria, yakiwa na uwazi na kuchochea ufanisi wa huduma kwa umma.
Bw. Shoo alieleza kuwa ushirikiano huu ni fursa ya kuendeleza ujumuishaji wa kidijitali katika sekta ya usafiri na akaahidi kuwa AzamPay iko tayari kushirikiana kwenye utekelezaji wa kiufundi na kibiashara.
Kikao kilihitimishwa kwa azimio la pamoja kuwa Mkataba wa Makubaliano (MoU) utakaoandaliwa ili kuweka msingi wa utekelezaji wa mradi huo, majukumu ya kila taasisi, na muda wa utekelezaji.
Mfungamanisho huu wa kadi unatarajiwa kuongeza urahisi wa malipo, kupunguza utegemezi wa pesa taslimu, na kuimarisha mwelekeo wa Tanzania kuelekea mfumo wa usafiri wa umma usio wa fedha taslimu.