News

​DART yaanzisha Kamati ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya fidia Awamu ya Pili.


Na Martha Komba

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umeanzisha Kamati ya kupokea na kushughulikia malalamiko kupitia mafunzo yake yenye lengo la kuwaelimisha wananchi wakati, kabla na baada ya kulipwa fidia kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka.

Mafunzo hayo yalianza kutolewa rasmi Mei 21,2018 katika Ofisi ya Kata ya Mianzini jijini Dar es Salaam na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka DART kwa kushirikiana na Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wakala wa Barabara Makao Makuu.

Katika mafunzo hayo wajumbe hao walifundishwa na kuelekezwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitu muhimu vya kuzingatia wakati wa ulipwaji fidia na namna gani mwananchi anaweza kujaza fomu ya malalamiko iwapo kuna tatizo lolote linalomkabili wakati na baada ya ulipwaji fidia.

“Tunajua kwa muda mrefu mmekuwa mkisubiri kulipwa fidia zenu ili kupisha ujenzi wa awamu ya pili ya miundo mbinu ya Mabasi Yaendayo Haraka. Serikali ipo pamoja nanyi na tunawahakikishieni kuwa haitapita miezi miwili bila kulipwa fidia hiyo kwani tupo katika hatua za mwisho za uhakiki tukishirikiana na Wizara ya Fedha,” alisema Mouston Mwakyoma ambaye ni Mthamini Mkuu wa DART.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu wa Wakala wa Barabara Makao Makuu Bi. Josephine Mwankusye alisema kuwa Serikali ina mapenzi mema na wananchi wake ndo maana imechukua jukumu la kuanzisha Kamati hiyo ya kupokea na kushughulikia malalamiko kwa lengo la kuondoa na kutatua kero zilizopo kuhusu masuala ya fidia.

Aliongeza kuwa katika uundwaji wa Kamati hiyo ya kupokea na kushughulikia malalamiko kwa ngazi ya Kata na mtaa watateuliwa viongozi watakaokuwa wanashughulikia malalamiko hayo kwa kushirikiana na DART upande wa Idara ya Maendeleo ya Usafirishaji. Viongozi hao watakaoteuliwa ni kutoka katika Mtaa na Kata ya Mianzini; Mtaa na Kata ya Kijichi na Mtaa na Kata ya Bora na Keko.

Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu wa DART Bi. Anna Gelle aliwaomba wananchi waishio Mbagala ambao maeneo yao yatapitiwa na ujenzi wa miundo mbinu ya Mabasi Yaendayo haraka, mara baada ya kulipwa tu fidia wajiandae kuondoka mapema ili kuepuka usumbufu wa kuondoka dakika ya mwisho hali ambayo itawasaidia kwenda kujipanga vizuri watakakokwenda.Pia watakuwa wameokoa vitu vingi kuliko kusubiri mpaka Serikali ichukue hatua ya kuwabomolea.

Akizungumzia suala la utaratibu katika ulipwaji fidia Afisa Ustawi wa Jamii Bi.Haikalel Mfangavo alisema kuwa kila mwananchi anatakiwa awe na vitu vifuatavyo muhimu ambavyo ni pamoja na barua ya utambulisho kutoka Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa husika; picha nne (4) za utambulisho, hati ya usimamizi wa mirathi endapo aliyeorodheshwa atakuwa amefariki; akaunti ya benki ambapo malipo hayo yatawekwa na sahihi ya mlipwaji kwenye jedwali la uthamini.

Mafunzo hayo ya kuunda Kamati ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya fidia yataendelea kutolewa kwa muda wa wiki moja na kila itakapotikana na nafasi Maafisa Ustawi wa jamii wataendelea kuelimisha viongozi walioteuliwa kushughulikia malalamiko hayo ili wawe na uelewa wa kutosha utakaowasaidia pia kuelimisha wananchi juu ya kujaza, kuandika na kuwasilisha Malalamiko hayo.

-Mwisho-

Tanzania Census 2022