News

DART yashiriki katika Maonesho ya Nane Nane, Mkoani Simiyu.


Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) iliyo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeshiriki maonesho ya Nane nane katika Viwanja vya Nyakabindi Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.

Katika banda la DART wananchi 650 waliweza kutembelea na kutoa maoni yao juu ya uboreshaji wa usafiri huo wa umma jijini Dar es Salaam.

Wageni waliofanikiwa kutembelea banda hilo ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Bw. Luhaga Joelson Mpina na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Bw. Jumanne A. Sagini.

Aidha, lengo kuu la DART kushiriki maonesho hayo ilikuwa ni kutoa elimu au uelewa juu ya mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka na mchango wake katika maendeleo ya Taifa letu. Kwa kutumia watumishi wake na dhana zingine za utoaji elimu kama vile vipeperushi na video, ili kutimiza lengo la kuhabarisha umma juu ya mradi wa DART.

Licha ya kutoa elimu juu ya mfumo, DART iliweza kupokea maoni, ushauri na pongezi za kutosha kutoka kwa wadau na wananchi waliokuwa na mwamko mkubwa wa kutembelea katika maonesho hayo na kuwaahidi kufanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa.

Tarehe 8 Agosti, mwaka huu ilikuwa kilele cha Sikukuu ya Nanenane na maadhimisho ya 25 ya Nanenane kwa mwaka 2018 katika Viwanja vya Nyakabindi, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu. Maonesho haya yanayowahusu wakulima na wafugaji wa Tanzania pamoja na wadau wao. Sherehe hizi za kila mwaka huangalia mafanikio na changamoto kwa wakulima na wafugaji kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa na kutafutia ufumbuzi wa matatizo hayo kwa wananchi.

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ikiwa moja ya idara chini ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilipata nafasi ya kushiriki maonesho hayo. DART ikiwa kama wakala wa serikali inayojihusisha na usafiri jijini Dar es Salaam imekuwa ni chachu ya maendeleo kwa kurahisisha hali ya usafiri na kukuza uchumi. Hivyo kwa kiwango kikubwa DART ilikuwa inaenda na kauli mbiu ya maonesho ya Nane Nane Simiyu ambayo ni Wekeza katika Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kwa maendeleo ya Viwanda”

Maonesho hayo ya Nane Nane yalifungwa na mgeni rasmi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, katika Viwanja vya Nyakabindi, Wilaya ya Bariadi, Mkoani Simiyu. Maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa miaka mitatu Mkoani Simiyu ili kuleta chachu ya maendeleo katika mkoa huo.

Tanzania Census 2022