Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Naibu Katibu Mkuu aitaka DART kuharakisha mawasiliano katika utwaaji wa maeneo ya BRT awamu ya tano
04 Aug, 2025
Naibu Katibu Mkuu aitaka DART kuharakisha mawasiliano katika utwaaji wa maeneo ya BRT awamu ya tano

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia miundombinu, Mha. Rogatus Mativila, ameielekeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART kuimarisha mawasiliano na wadau wote kabla ya kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Tano ya BRT.

Mha. Mativila alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Agosti 1, 2025 ambapo viongozi wa TAMISEMI wakiambatana na Menejimenti ya DART na maafisa wengine wa Wakala walitembelea maeneo yaliyoainishwa kwa ajili ya ujenzi wa karakana za Awamu ya Tano.

Katika ziara hiyo rasmi kutoka Dodoma, Mha. Mativila aliambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miundombinu wa TAMISEMI, Mha. Gilbert Moga, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji, Mha. Ezron Kilamhama, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu, Dkt. Philemon Mzee, na maafisa waandamizi akiwemo Bi. Delfina Pwereza, Bi. Albina John, Muston Mwakyoma pamoja na maafisa wengine wa DART.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa kuwaonyesha viongozi wa TAMISEMI maeneo muhimu yaliyoainishwa kwa ajili ya ujenzi wa karakana za Awamu ya Tano, ambazo zitakuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa mradi huo.

Maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Ubungo Maziwa, ambapo karakana mpya itajengwa kuchukua nafasi ya karakana ya Jangwani iliyobomolewa katika Awamu ya Kwanza. Maeneo mengine ni eneo la NHIF kwa ajili ya karakana ya Awamu ya Tano, eneo la Sigara Tabata-Segerea, na eneo karibu na Uwanja wa Taifa litakalotumika kwa karakana nyingine ya Awamu ya Tano.

Akihitimisha ziara hiyo, Mha. Mativila aliitaka DART kuhakikisha inashirikisha wadau wote wanaohusika na maeneo hayo kabla ya kupeleka maombi kwa TAMISEMI ya kupata msaada wa kuyamiliki maeneo husika.

“DART lazima ifanye maandalizi ya awali kwa kushirikisha wadau wote badala ya kutuma barua za maombi kwa wizara na kusubiri hatua kuchukuliwa,” alisisitiza Mha. Mativila.

Amehimiza mawasiliano ya moja kwa moja na wamiliki wa ardhi, mamlaka za mitaa, na taasisi husika ili kuepusha ucheleweshaji wa ujenzi wa miundombinu.

Pia, Mha. Mativila alitoa agizo kwa DART kuondoa mara moja watu wote waliolipwa fidia kwa mali zao ili kuepusha hatari ya mali hizo kuuzwa tena na kuleta mgogoro.

Alipongeza jitihada za DART katika utekelezaji wa awamu zilizopita za mradi wa BRT na kusisitiza dhamira ya Serikali katika kuunga mkono ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wake, Mha. Ezron Kilamhama, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafiri, alimhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa DART itaongeza juhudi za mawasiliano na uratibu ili kutekeleza maagizo hayo.

Dkt. Philemon Mzee, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu, alieleza kuwa tayari DART imeanza mazungumzo na wadau wa maeneo husika ili kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa DART aliyeshiriki kwenye ziara hiyo alisema Wakala umejipanga kuhakikisha taarifa zote muhimu kuhusu maeneo yaliyotengwa zinafikishwa ipasavyo kwa umma na taasisi husika.