Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Ujenzi wa Mradi wa DART Awamu ya Tatu
28 Aug, 2023
Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Ujenzi wa Mradi wa DART Awamu ya Tatu

Kamati ya kudumu ya bunge ya TAMISEMI, imeeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya Tatu inayoendelea kujengwa katika Barabara ya Nyerere kuelekea Gongolamboto, na kuelekeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kumsimamia kwa ukaribu Mkandarasi ili aweze kumaliza kazi hiyo kwa wakati.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua miundombinu hiyo ya Awamu ya Tatu, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya hiyo Mhe. Justin Nyamoga alisema japo kazi inayoendelea ni nzuri na inaendelea kwa kasi ni vyema DART ikaongeza nguvu zaidi katika usimamizi ili kazi ikamilike kwa muda uliopangwa na iwe katika viwango vya ubora unaohitajika.

“Kukamilisha kazi ni jambo moja lakini ubora ni jambo lingine, kamati inaelekeza DART kuhakikisha inasimamia ubora wa kazi unaoendana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa, Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawategemea sana kuhakikisha miundombinu hii inakamilika kwa viwango vya kimataifa hivyo msimwangushe” Alisema Mhe. Nyamoga.

Aidha, Mhe. Nyamoga alitaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka kuharakisha mchakato wa ununuzi wa Mabasi ili kuwaondolea adha ya usafiri wakazi wa Dar es Salaam ambao kwa kipindi hiki ambacho Mabasi hayatoshi wanaona kama Serikali yao haiwajali.

Sambamba na maelekezo hayo Makamu Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge alielekeza pia DART kukamilisha kwa haraka mfumo wa kadi janja( smart card) ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali lakini pia kuwaondolea abiria usumbufu wa kutumia tiketi za karatasi.

Kamati pia iliupongeza Wakala wa DART kwa kutumia wataalam wa ndani ya nchi katika kutenegeza na kusimamia mifumo ya tehama jambo ambalo sio tu la kizalendo bali linaleta heshima kwa nchi.

Kwa upande wake mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Magreth Sitta alishauri serikali kuwa na utamaduni wa kutenga maeneo ya kujenga miundombinu kama ya BRT mapema kabla ya kuanza ujenzi ili kuepuka ulipaji wa fidia jambo ambalo linachelewesha ujenzi wa miradi na pia linaongeza gharama.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Edwin Mhede alisema kwa sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 17.6 na kwamba mkandarasi yuko nje ya muda na ameelekezwa kufanya jitihada kumaliza kwa wakati.

“Mhe. Mwenyekiti mkandarasi katika ujenzi huu yuko nyuma ya muda kwa asilimia 3 tumemwelekeza kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia malengo, na sisi tutambana kweli kweli kuhakikisha anakamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba” Alisema Dkt. Mhede.

Akizungumzia changamoto ya vumbi kwa wakazi wa eneo mradi unakotekelezwa Dkt.Mhede alisema wanaendelea kumsimamia na kumwelekeza mkandarasi kumwaga maji kila siku ili kupunguza vumbi kwani ni chanzo cha magonjwa kwa wakazi wa pembezoni mwa Barabara ya Nyerere ambako ujenzi huo unaendelea.

Mradi huo wa BRT awamu ya Tatu unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka 2024, ambapo utakuwa kichocheo cha uchumi kwa wakazi wa Gongolamboto na maeneo ya jirahi hadi katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Akizungumzia suala la kuongeza idadi ya Mabasi Dkt.Mhede alisema Wakala umejipanga kuhakikisha adha hiyo inakwisha na mchakato wa kupata Mabasi unaendelea vyema hivyo wananchi waendelee kuiamini serikali yao kwani inafanyia kazi changamoto hiyo.