Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Bodi yahimiza kukamilisha ujenzi wa kituo cha Kivukoni kabla ya kuanza kwa huduma ya mabasi ya Awamu ya Pili
22 Aug, 2025
Bodi yahimiza kukamilisha ujenzi wa kituo cha Kivukoni kabla ya kuanza kwa huduma ya mabasi ya Awamu ya Pili

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dkt. Florence Turuka, ameagiza kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Kivukoni kabla ya mwisho wa Agosti 2025 ili kuhakikisha huduma za mabasi ya Awamu ya Pili kupitia Barabara ya Kilwa zinaanza kwa wakati.

Agizo hilo lilitolewa wakati wa kikao cha siku tatu cha Bodi kilichofanyika kuanzia Agosti 18 hadi Agosti 20, 2025, katika ofisi za Wakala wa DART. Kikao kilihusisha uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa robo ya tatu na ya nne, na siku ya mwisho ilihitimishwa kwa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi.

Katika ziara ya Agosti 20, wajumbe wa MAB pamoja na Menejimenti ya DART walikagua maeneo matatu muhimu: mabasi 99 mapya bandarini Dar es Salaam, usimikaji wa vifaa vya gesi asilia (CNG) katika karakana ya Mbagala, na Kituo cha Kivukoni ambacho kiko katika hatua za mwisho za ujenzi.

Mabasi hayo kutoka Kampuni ya Mofat, yameletwa kwa ajili ya kutoa huduma katika Awamu ya Pili inayopita Barabara ya Kilwa. Bodi ilielezea kuridhishwa na maendeleo hayo, lakini ikasisitiza umuhimu wa kukamilisha kazi za miundombinu kwa wakati.

Katika karakana ya Mbagala, wajumbe walishuhudia kazi zinazoendelea za usimikaji wa vifaa vya kujaza gesi asilia (CNG) vinavyosimamiwa na Kampuni ya Lake Oil Ltd. kwa ajili ya mabasi mapya ya Awamu ya Pili.

Wakiwa katika Kituo cha Kivukoni, wajumbe walijadili masuala mbalimbali ikiwemo iwapo wauzaji wa samaki wa eneo la Feri wataruhusiwa kubeba mizigo yao kwenye mabasi, na uwezekano wa kuwa na mabasi maalum kwa abiria wa wenye uwezo wa kifedha, na kwa viwango tofauti vya nauli.

Mhandisi Ezron Kilamhama, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji katika Wakala wa DART, alieleza kuwa Kituo cha Kivukoni kina sehemu nne: “Sehemu ya kwanza ni kwa Awamu ya Kwanza (Kimara, Morocco na Gerezani); sehemu ya pili kwa Awamu ya Pili (Mbagala); sehemu ya tatu ni kwa Awamu ya Tatu (Gongolamboto kupitia Nyerere); na sehemu ya nne ni kwa ajili ya Awamu ya Nne (Tegeta kupitia Bagamoyo),” alieleza.

Mkandarasi wa mradi alieleza kuwa kuna kipande kidogo cha barabara ya Awamu ya Pili ambacho hakijakamilika. Dkt. Turuka aliagiza Wakala wa DART kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuzuia ucheleweshaji wa huduma.

Dkt. Athumani Kihamia, Mtendaji Mkuu wa DART, alihakikishia wajumbe kuwa kazi zote za miundombinu, gesi, na mifumo ya tiketi zitakamilika kwa wakati. “Tunaendelea kushirikiana na wakandarasi na wadau kuhakikisha huduma za Awamu ya Pili zinaanza bila changamoto,” alisema.

Wajumbe pia walikagua vituo vya abiria vya barabara ya Kilwa, maandalizi ya njia za mlisho, na ujumuishaji wa mfumo wa kadi ya Mwendokasi na mageti ya kielektroniki (AFCS).

Dkt. Turuka aliipongeza DART kwa hatua kubwa iliyofikia katika ununuzi wa mabasi na miundombinu, lakini akasisitiza umuhimu wa mawasiliano ya wazi kwa wadau, hususan wauzaji wa bidhaa ndogondogo na mamlaka za serikali za mitaa.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuratibu vipengele vyote vya uendeshaji — kuanzia maandalizi ya barabara, miundombinu ya gesi, elimu kwa umma, hadi mifumo ya tiketi — kwa mafanikio ya uzinduzi wa Awamu ya Pili.