News

Mabadiliko ya mwelekeo wa fikra ndani ya mabasi ya DART yapaswa kufanyikaWazo la kuanzisha mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka au kwa jina maarufu la Kiingereza ‘Bus Rapid Transit (BRT) katika Jiji la Dar es Salaam limetokana na kuongezeka kwa msongamano wa magari kila kukicha huku idadi ya watu ikizidi kuongezeka kwa kasi katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita. Vilevile, msongamano huo umeendana na kuongezeka kwa idadi ya watu kumiliki magari binafsi kwa ajili ya kwenda na kurudi katika shughuli zao kama makazini au sehemu za biashara badala ya kutumia usafiri wa umma.

Mwelekeo wa watu kutumia magari yao kwenda ofisini au sehemu za biashara katika jiji linalochangia kiasi kikubwa cha pato la taifa kiuchumi umetokana na hali ya usafiri wa umma kuwa hafifu kutokana na watumiaji wa usafiri wa umma kujikuta wanatumia muda mrefu kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine hasa wakati wa asubuhi na jioni ambapo watu wengi husafiri.

Katika mfumo wa kawaida wa usafiri wa umma ambao umekuwa ukitumia mabasi madogo yajulikanayo kwa jina maarufu ‘daladala’, wasafiri kwa mabasi hayo wamekuwa wakitumia muda mrefu takribani saa mbili na nusu au zaidi kabla ya kufika katika vituo husika kwasababu ya ongezeko kubwa la magari na idadi ya wakazi wa jiji na miundombinu isiyotosha na mingine kuwa na hali mbaya.

Ili kuboresha usafiri wa umma Jijjini Dar es Salaam, kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2000 Serikali ya Tanzania iliamua kuanza kutekeleza mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na baadae kuanzishwa kwa Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka mwaka 2008 ili kuongeza ufanisi wa kusimamia mradi huo chini ya Ofisi ya Rais (Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa).

Lengo kubwa la kuanzisha mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni kusafirisha watu wengi kwa wakati mmoja ili kuwawezesha watumiaji wa mfumo huo kufika haraka kule wanapokwenda. Hivyo, ili watu wengi wafike mapema katika sehemu zao za kazi au biashara, mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 140 na mengine hadi watu 80 yanatumika kwa kutumia njia maalumu ili kupunguza msongamano na kushawishi watu kuacha kutumia magari yao.

Dhana ya mabasi makubwa kuwa na viti vichache ni kuwawezesha abiria wengi kuingia katika Basi moja huku ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya watu waliomo katika Basi hilo wawe wamesimama na wengine wachache wawe wamekaa katika viti. Idadi ndogo ya viti vilivyopo katika mabasi ya DART ni kwa ajili ya makundi maalum kama vile wazee, watu walio na ulemavu, wagonjwa, na wajawazito, na akinamama au baba wenye watoto wadogo.

Idadi kubwa ya abiria ndani ya Basi wakiwa wamesimama ni utaratibu ambao unatumika duniani kote ambako miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka hutekelezwa.

Kuanzishwa kwa huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka katika kipindi cha mpito mnamo Mei 10, 2016 kumeleta mwamko wa watu wengi kupenda kutumia mabasi ya DART. Kama huduma za mabasi ya DART zinatolewa vizuri, watu wamejifunza kuwa kwa kutumia usafiri huu wanaweza kutumia muda mfupi sana kufika ofisini au sehemu zao za biashara badala ya kutumia daladala ambapo wangetumia zaidi ya saa mbili na nusu kutoka Kimara hadi Kivukoni. Kwa kutumia mabasi ya DART sasa wanaweza kutumia dakika 40 tu.

Jambo la kushangaza katika usafiri wa umma kwa kutumia mabasi ya DART, watu wengi wanapenda wapate kiti cha kukaa na hawapendi kusimama. Kutokana na mwelekeo fikra huu, watu wengi wanaosubiria mabasi katika vituo mbalimbali huanza kugombania kuingia katika basi kwa malengo ya kupata kiti ili wakae hata kama wao sio wagonjwa, wazee, wenye ulemavu, au wajawazito.

Kutokana na mwelekeo fikra wa namna hii, utashangaa kuona watu wengi ambao walikuwa wanasubiria basi kufika katika kituo husika wamesusia kuingia kwenye basi eti kwa sababu tu hawajapata kiti. Hivyo, tabia ya namna hii husababisha msongamano wa watu katika vituo wakisubiri Basi lingine lije katika kituo hicho. Endapo watakosa kiti tena watu hao huendelea kusubiri basi lingine huku wakianza kulaani kuwa mabasi ni machache mno na kusema wanakaa muda mrefu kwenye vituo.

Mabasi hayo yametengenezwa kwa ajili ya kubeba watu wakiwa wamesimama ikitegemewa kuwa urefu wa safari za usafiri wa umma katika miji mikubwa ni mfupi na hivyo mtu hategemewi kupata madhara ya kiafya yatokanayo na kusimama kama ilivyo katika usafiri wa mabasi ya mikoani ambayo ni wa masafa marefu.

Katika tabia hiyo ya kutaka kukaa kwenye kiti wakati ukisafiri na mabasi ya DART, watu wengi wameonekana hata kudiriki kupanda mabasi hayo katika vituo vya njiani ili mtu huyo aanze kuulizia kama kuna baadhi ya abiria waliokaa kwenye viti wana mpango wa kushuka katika kituo cha mwisho ili waweze kujipatia kiti kabla ya abiria walioko katika kituo husika hawajaingia ndani ya basi hilo.

Ili tuweze kufurahia usafiri wa DART wananchi wote yatupasa kubadili mwelekeo wa fikra wa mambo mbalimbali yahusuyo kutumia mabasi hayo ikiwemo kutaka kupata kiti ndani ya mabasi hata kama mtu hana kasoro yoyote kiafya. Wananchi wanapaswa kubadili mtizamo ili kuhakikisha miundombinu iliyopo katika vituo na hata mabasi inadumu kwani kwasasa kuna uharibifu umeendelea kutokea kutokana na watu kutofuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kugombania na kuingilia madirishani.

Kila mmoja wetu ajiulize ikiwa kila abiria anapaswa kupata kiti ndani ya Basi la DART wakati kuna watu, mathalani, elfu nne katika kituo wakisubiri usafiri kuelekea sehemu mbalimbali za Jiji, tungepaswa kuagiza mabasi mengi sana ambayo kila Basi lina uwezo wa kuwa viti 65 kama yale yanayotoa huduma kwenda mikoani. Kwa mtazamo huo tungepaswa kuwa na idadi kubwa sana ya mabasi ili kuwezesha watu wasafiri na DART na hivyo kuleta tatizo lingine la msongamano la mabasi ya DART katika jiji la Dar es Salaam na kuhitajika uwekezaji mkubwa zaidi kwa mabasi hayo mengi ambapo itasababisha kuwa na nauli kubwa.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Faustine Kamuzora akiwa katika ziara ya kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa DART, ameshangazwa kuona watu wakigombania viti katika mabasi ya DART.

Katibu Mkuu huyo amesistiza umuhimu wa kuwekeza katika kuwaelimisha watu kuhusu matumiziya usafiri wa BRT na kuondokana na dhana potovu kuwa abiria lazima apate kiti anapoingia kwenye Basi.

Prof. Kamuzora amehimiza pia kuwa usafiri wa DART sio kwa ajili ya kusafirisha watu wengi kwa muda mfupi pekeyake bali usafiri wa DART ni kwa ajili ya kuboresha ustaarabu wa watumiaji wa mfumo huo kwa kuondokana na desturi za zamani kwa watu wenye uwezo wa fedha kutaka kuendesha magari binafsi kila wanakokwenda.

Amesema kuwa wakati umefika ambapo wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanapaswa kuthamini mradi wa DART na kupenda kufuata maelekezo ya namna mradi huo unavyowapasa kuutumia ili kuufurahia na kuleta tija zaidi katika maisha yao na wawekezaji katika mradi huo.

Mhandisi Ronald M. Lwakatare

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)

Dar es Salaam, Tanzania.

Tanzania Census 2022