Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Waziri Mchengerwa atoa wito kwa DART kutanua wigo wa huduma maeneo mengine
24 Oct, 2023
Waziri Mchengerwa atoa wito kwa DART kutanua wigo wa huduma maeneo mengine

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuwa wabunifu kwa kuongeza mtandao wa miundombinu.

Mheshimiwa Mchengerwa ametoa wito huo Oktoba 24, 2023 wakati alipotembelea DART kufahamu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka.

Waziri Mchengerwa ametembelea DART ikiwa ni ziara yake ya kwanza kwa Wakala tangu kuteuliwa kwake Septemba 1,2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Aidha, Mheshimiwa Mchengerwa ameongeza kuwa DART ni lazima iongeze Mtoa huduma ya mabasi zaidi ya mmoja ili kuleta ushindani katika Awamu ya Kwanza Mradi ambako huduma inatolewa na awamu nyingine zitakazofuata ili Mradi uweze kufikia malengo kusudiwa.

“Ni wakati muafaka kwa DART kutafuta uwezekano wa kuwa na mtoa huduma zaidi ya mmoja ili huduma zinazotolewa ziweze kukidhi viwango vilivyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Sita na Watanzania waweze kufurahia huduma zinazotolewa na Wakala katika Jiji la Dar es Salaam.” Amesema Mchengerwa

Vilevile Mheshimiwa Mchengerwa alitoa maagizo kwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI kuharakisha mchakato wa utungwaji wa Sheria ya DART ili kuwezesha Wakala huo kutanua wigo wa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka nje ya Mkoa Dar es salaam.

Naye Mtendaji Mkuu wa DART), Dr. Edwin Mhede alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa ujio wake DART na kwamba alimuhakikishia kuwa Serikali kupitia Wakala inafanya juhudi kuhakikisha katika kipindi kifupi kijacho mabasi yatakuwa ya kutosha na wananchi watafurahia na kunufaika na huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka.