Kamati ya Bunge yapongeza kasi ya ujenzi awamu ya tatu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imepongeza maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu katika Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, ikieleza kuwa mradi huo uko karibu kukamilika na utaboresha huduma za usafiri wa umma katika jiji hilo.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 14, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanyika katika Kituo Kikuu cha Gongolamboto, ambapo wajumbe wa kamati walikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wenye urefu wa takribani kilomita 23.3 kutoka katikati ya jiji hadi Gongolamboto.
Ziara hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa mradi wa BRT wakiwemo maafisa kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi.
TANROADS ambayo ina jukumu la kusimamia ujenzi wa barabara pamoja na miundombinu ya vituo vya BRT ndiyo iliyokuwa mwenyeji wa ziara hiyo na kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Taarifa hiyo ya maendeleo iliwasilishwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu TANROADS. Katika uwasilishaji wake alieleza hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
Kulingana na taarifa ya Mhandisi Mlavi, ujenzi wa miundombinu ya BRT Awamu ya Tatu umefikia takribani asilimia 99 ya utekelezaji, hali inayoonesha kuwa mradi huo uko katika hatua za mwisho za kukamilika.
Wajumbe wa kamati walieleza kuridhishwa na kasi pamoja na ubora wa kazi iliyofanyika, wakibainisha kuwa maendeleo hayo yanaonesha jitihada kubwa za Serikali pamoja na taasisi zinazotekeleza mradi huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Seleman Kakoso, aliwapongeza wadau wote kwa maendeleo yaliyofikiwa na kuwataka kuhakikisha kuwa kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati uliopangwa.
Alitoa maelekezo kwa Wakala wa DART kuhakikisha maandalizi ya uendeshaji wa mabasi yanafanyika mapema ili huduma za mabasi zianze mara tu miundombinu ya mradi itakapokamilika rasmi.
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega, ambaye aliambatana na kamati hiyo katika ziara hiyo, alipokea maelekezo yaliyotolewa na kamati na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha yanatekelezwa kwa wakati.
Alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mradi wa BRT Awamu ya Tatu unaanza kutoa huduma kwa wakati uliopangwa ili kuboresha usafiri wa wananchi na kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Gongolamboto, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka- DART, Bw. Said Tunda, aliahidi kuwa wakala huo utachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kuwa huduma za mabasi zinaanza kwa wakati mara tu miundombinu itakapokamilika.
