Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Mfumo wa ukusanyaji nauli wa DART kuigwa na mkoa wa Dar es Salaam
17 Aug, 2023
Mfumo wa ukusanyaji nauli wa DART kuigwa na mkoa wa Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Daressalaam, Mhe. Albert Chalamila yuko katika hatua ya kukaribisha wataalam wa TEHAMA katika harakati za kutengeneza mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na mkoa wake kufuatilia makusanyo ya mapato katika halmashauri za mkoa huo.

Chalamila amefikiria kuchukua uamuzi huo wakati akizungumza na  Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) katika ziara ambayo ameifanya Alhamis, Agosti 17,2023 katika ofisi za Wakala Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa huyo  ameusifu Wakala wa DART kwa kutengeneza Mfumo wa kukusanya nauli,Automated Fare Collection System (AFCS) ambao pia watumiaji wa mfumo huo wanaweza kukusanya nauli na kufuatilia kiasi kinachokusanywa kwa kila kituo hivyo kusaidia kudhibiti upotevu wa mapato.

Aidha, Chalamila ameutaka Wakala kutoa ushirikiano na mkoa wake katika kuunda mfumo unaofanana na mfumo wa kukusanya nauli wa DART ili uweze kutumiwa kudhibiti mapato katika mkoa wake.

Vilevile, Chalamila ameupongeza Wakala huo kwa kusimamia vyema mradi huo kwani umebeba taswira ya Taifa hususan kwenye sekta ya kiuchumi na maendeleo ya usafirishaji.

Akiweka mkazo umuhimu wa taasisi za Serikali kuwa na ushirikiano katika miradi ya kimkakati hususan usafirishaji, Chalamila amesema kuwa DART, Wakala wa Barabara (TANROADS)  pamoja na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA wanapaswa kushirikishana mipango na taarifa mbalimbali za miradi ili kuimarisha sekta ya usafiri wa umma nchini.

Hata hivyo, Chalamila ametaja uwepo wa changamoto mbalimbali katika mradi wa DART ikiwemo uhaba wa idadi ya mabasi kitu ambacho kinaakisi uhitaji mkubwa wa usafiri huo wa umma kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam na wageni wanaotembelea Jiji hilo.

Ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa ilikuwa ni sehemu ya matayarisho yake kwa ziara atakazozifanya kwa kina katika mradi huo ikiwemo kutembelea  Awamu ya Kwanza na Awamu nyingine ambazo ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.