News

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla aipongeza DART


Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Mhe Amos Makalla ameupongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwa kusimamia vyema ujenzi wa miundombinu hasa katika barabara ya Kilwa ambako awamu ya Pili ya mradi inaendelea kujengwa.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam Mh.Makalla amesema wananchi wanasubiri kwa hamu kubwa kukamilika kwa ujenzi ili hatimaye huduma za usafiri zianze.

“Nimeridhishwa na jitihada zinazofanywa na DART katika kusimamia ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka, nasisitiza muhakikishe ujenzi unakamilika kwa wakati ili wananchi wa Mbagala waanze kunufaika na uwekezaji unaofanywa na serikali yao” Alisema.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Mh. Dr. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo sekta ya usafiri wa umma.

Mh.Makala amempongeza pia mkandarasi anayeendelea na ujenzi wa BRT awamu ya Pili Sino Hydro Cooperation kwa kazi inayoendelea kufanyikalicha ya changamoto mbalimbalizinazojitokeza, zikiwemo zile za baadhi ya wananchi ambao wamelipwa fidia kugoma kuhama ili kupisha ujenzi wa mradi.

Ujenzi wa miundombinu katika awamu ya Piliya BRT kwa sasa umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilikamwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2023.

Mkuu wa Mkoa amewasisitiza wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano kwa DART wakati wanaendelea na usimamizi wa ujenzi wa miundombinu kwa kuhakikisha huduma muhimu za umeme, maji na usalama wa uhakika vinakuwepo ili mradi ukamilike kwa wakati.

Makalla amewaonya wananchi,wafanyabiashara ndogo ndogo na vyombo wa usafiri kuacha mara moja kukatiza na kufanya shughuli katika miundombinu ya BRT inayoendelea kujengwa,na amewaagiza Katibu Tawala na Mkurugenzi kuwahamisha mara moja wafanya biashara wanaofanya biashara katika maeneoambapo ujenzi unaendelea.

Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unatekelezwa katika awamu sita,Awamu ya Kwanza ambayo imeshakamilika na inaendelea na huduma ni barabara yenye urefu wa kilomita 20.9 ikihusisha barabara ya Morogoro(Kimara-Kivukoni),Kawawa(Morocco-Magomeni) na Msimbazi,Fire hadi Kariakoo.

Awamu ya Pili ya Mradi inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Machi mwaka huu ina urefu wa kilomita 20.3 inahusisha barabara za Kilwa,kawawa hadi Mbagala Rangitatu,Gerezani na Chang’ombe.