Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Waziri Mkuu aagiza kuanza haraka kwa huduma za BRT awamu ya pili
15 Aug, 2025
Waziri Mkuu aagiza kuanza haraka kwa huduma za BRT awamu ya pili

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezielekeza taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kuharakisha maandalizi ya mwisho ili huduma za Awamu ya Pili zianze rasmi kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika katika makazi yake Mikocheni, Dar es Salaam, akiwa na Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athumani Kihamia, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wakala na maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kikao hicho kilijadili hali ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mradi inayopita barabara ya Kilwa hadi Mbagala Rangi Tatu. Ilielezwa kuwa mabasi 99 ya gesi asilia (CNG) kutoka Kampuni ya Mofat tayari yamewasili bandarini Dar es Salaam, yakisubiri taratibu za mwisho za uthibitisho na ushuru kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA.

Dkt. Kihamia alieleza kuwa mabasi mengine 52 tayari yamesafirishwa kwa meli, na mengine yatawasili kwa awamu hadi kukamilisha mabasi yote 255 yanayotarajiwa kutolewa na Mofat kwa huduma ya njia kuu (trunk) ya Awamu ya Pili.

Aidha, alitoa taarifa kuwa kampuni mbili za huduma za njia za mlisho (feeder) — Metro City Company Limited na YK City Link — zinatarajiwa kuleta mabasi kwa ajili ya maeneo ya Mbagala na vitongoji vyake. Metro City italeta mabasi 334, huku YK City Link ikileta mabasi 116 kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Waziri Mkuu alionesha nia ya kutembelea bandari ili kukagua mabasi hayo na kuona maendeleo ya hatua za usimikaji wa miundombinu ya gesi asilia (CNG) yanayoendelea kufanywa na Lake Oil Company Ltd. katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu.

Pia alipokea taarifa kuhusu Mfumo wa Ukusanyaji Nauli wa Kielektroniki (AFCS), hususan usimikaji wa mageti ya kisasa katika vituo vyote vya mabasi. Alisisitiza kuwa mfumo huo lazima ukamilike kabla ya kuanza kwa huduma rasmi.

Mhe. Majaliwa aliielekeza mamlaka yenye kuhusika na kutangaza viwango vya nauli -LATRA, itangaze viwango vipya vya nauli za BRT mara moja, na kuwaeleza wananchi sababu za msingi za mabadiliko hayo, ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji wa mabasi ya kisasa.

“Nauli lazima iendane na ubora wa huduma. Lakini lazima pia ielezwe kwa wananchi kwa uwazi. Tunahitaji kuungwa mkono na uelewa wa umma,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Dkt. Zanifa Omary, Mkurugenzi wa TEHAMA wa DART, alisema kuwa mfumo wa AFCS utatumia kadi ya Mwendokasi, ambapo abiria watachanja ili kuingia na kutoka, huku taarifa zote za miamala zikitunzwa wakati huohuo. “Tuko hatua za mwisho za kuunganisha mifumo ya watoa huduma,” alisema.

Kwa upande wa uendeshaji, Dkt. Philemon Mzee, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu, alieleza kuwa mabasi ya Mofat yatahudumia njia kuu kutoka Mbagala hadi Kivukoni, huku mabasi ya feeder kutoka Metro City na YK City Link yakitoa huduma katika maeneo ya Chamazi, Kigamboni, na sehemu zilizo kandokanzo ya Mbagala.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa kadi ya Mwendokasi lazima itumike badala ya tiketi za karatasi, akisema: “Mfumo wa karatasi umepitwa na wakati. Mfumo wa kielektroniki unaongeza ufanisi na uwazi wa mapato.”

Kikao kilithibitisha kuwa huduma za Awamu ya Kwanza kupitia barabara ya Morogoro chini ya kampuni ya TransDar zitaanza mwezi Oktoba 2025 kwa mabasi 177 ya dizeli ya kiwango cha Euro 6.

Waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jimmy Yonas, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, na viongozi wengine waandamizi.

Dkt. Athumani Kihamia, Mtendaji Mkuu wa DART, alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa taasisi yake iko tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha huduma za Awamu ya Pili zinaanza kwa wakati na kwa mafanikio.