Mkuu wa Mkoa aipongeza DART kwa utekelezaji wa mradi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amefanya ziara katika ofisi za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) unaotekelezwa kwa awamu sita jijini Dar es Salaam, na kupongeza DART kwa juhudi za kuongeza Mabasi ili kuondoa kero ya usafiri wa umma mijini.
Mh. Chalamila katika ziara hiyo alimbatana na kamati ya usalama ya Mkoa ambapo walielezwa namna ambavyo Wakala unashughulikia kero ya uchache wa Mabasi na hatua mbalimbali ambazo Wakala umezichukua ili kutatua changamoto hiyo, pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu na maandalizi ya kuanza kwa huduma za mabasi kwa Awamu ya Kwanza na ya Pili.
Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Athumani Kihamia aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, ambayo ni Awamu ya Kwanza kutoka Kimara hadi Kivukoni kupitia barabara ya Morogoro, Magomeni Mapipa hadi Morocco kupitia barabara ya Kawawa, na kutoka Fire hadi kituo kikuu cha Gerezani kupitia barabara ya Msimbazi, yenye jumla ya kilomita 20.9.
Dkt. Kihamia ameeleza kuwa kwa Awamu ya Kwanza, DART imesaini mkataba na kampuni ya Emirates National Group ENG kama Mtoa huduma ambaye ataleta Mabasi 177 yanayotumia mafuta ya dizeli aina ya Euro 3, ambayo yanatarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Oktoba 2025.
Kwa upande wa Awamu ya Pili inayopita barabara ya Kilwa hadi Mbagala, DART imesaini mikataba na kampuni tatu, ikiwemo kampuni ya Mofat Company Limited kwa ajili ya njia kuu (trunk routes).
Aidha, Dkt Kihamia alieleza kuwa tayari Mabasi mapya 99 yamepakiwa kwenye meli nchini China ambayo yanatarajiwa kuwasili mwezi Agosti.
Dkt. Kihamia amesisitiza kuwa DART imejipanga kuhakikisha uendelevu wa mazingira kwa kutumia mabasi yanayotumia gesi asilia katika Awamu ya Pili, na kuanzia Awamu ya Tatu hadi ya Sita, mabasi yote yatakuwa yanatumia nishati ya umeme.