Mkuu wa Mkoa aagiza kuanza kwa huduma ya mabasi awamu ya pili
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila leo, Novemba 18 aliongoza wadau wa usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka-BRT kukagua miundombinu ya Mwendokasi iliyoharibiwa katika Awamu ya Pili kuanzia Kituo cha Bandari hadi Mbagala Zakhem, katika barabara ya Kilwa.
Wakati wa ukaguzi, Mkuu wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya umma, akibainisha kuwa miundombinu ya BRT ni mali ya wananchi na ilianzishwa ili kuboresha usafiri na maisha ya wakazi wa Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, walikuwepo Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Philemon Mzee, watendaji waandamizi wa DART, maafisa kutoka LATRA, UDART, MOFAT, Jeshi la Polisi pamoja na waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia juhudi za urejeshaji wa huduma.
Bwana Chalamila alimwomba Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, kutoa taarifa kuhusu maoni ya wananchi juu ya uharibifu huo. Mhe. Mapunda alieleza kuwa wananchi wa Temeke walikuwa wamesikitishwa na vitendo vya uharibifu na walitaka huduma za usafiri zirudi haraka iwezekanavyo.
Mhe. Mapunda aliongeza kuwa uharibifu wa miundombinu ya BRT uliathiri maisha ya watu waliokuwa wakitegemea mfumo huo katika shughuli zao za kila siku.
Baada ya maelezo hayo, Bwana Chalamila aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuthamini na kulinda miradi ya maendeleo ikiwemo BRT kwa kuwa ni mali yao na inachangia ustawi wa jamii.
Alichukua nafasi hiyo kusisitiza kuwa endapo kungekuwa na malalamiko dhidi ya serikali, njia sahihi ingekuwa kukaa meza moja kwa ajili ya suluhu badala ya kuharibu miradi ya umma ambayo hatimaye huwaumiza wananchi wenyewe.
Baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wahandisi wa DART, Mkuu wa Mkoa alielezwa kuwa uharibifu katika Awamu ya Pili ulikuwa mdogo ukilinganisha na Awamu ya Kwanza ambayo ilipata madhara makubwa kwenye vituo, njia maalum na mifumo ya TEHAMA.
Hivyo, Bwana Challamila aliagiza DART kuanza huduma ya mabasi Awamu ya Pili kuanzia Novemba 20 bila kuacha, akisisitiza kuwa wananchi walihitaji huduma hiyo kwa haraka.
Kwa mujibu wa Dkt. Mzee, huduma ya awali ya mabasi Awamu ya Pili zitakuwa zinatolewa kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku kila siku wakati ukarabati ukiendelea kwenye vituo vilivyoharibika.
Wakala wa DART ulisisitiza dhamira yake ya kushirikiana na serikali, vyombo vya ulinzi na watoa huduma ili kuhakikisha huduma za usafiri za mabasi yaendayo haraka zinarejea salama na kwa ufanisi huku ikijenga upya imani ya wananchi.
