News

Ujenzi wa miundombinu ya DART Mbagala kuanza karibuni


UJENZI WA MIUNDO MBINU YA DART MBAGALA KUANZA KARIBUNI

Na Martha Komba

Baadhi ya wananchi wa Mbagala ambao walikuwa bado hawajaridhia kupisha ujenzi wa miundo ya DART wameridhia ili ujenzi huo uendelee.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana baada ya kikao kilichofanyika katika Ofisi za Mtendaji wa Kata Mianzini baina ya wananchi hao na wataalaam wa DART wakishirikiana na watalaam wa Manispaa ya Temeke.

Katika vikao mbalimbali vilivyofanyika katika ofisi hiyo ya Mianzini kuna baadhi ya wananchi walikuwa bado hawajaridhia uamuzi wa kupisha ujenzi wa miundo mbinu hiyo ya DART.

Mara baada ya wataalam wa DART na Manispaa ya Temeke kuongea na wananchi hao na kuwaeleza sheria na kanuni za ulipwaji wa fidia na kwamba hakuna mwananchi ambaye atanyimwa haki yake, wananchi hao waliridhika na maelezo hayo na kukubaliana ujenzi wa miundo mbinu uanze ili wananchi waweze kupata usafiri wa haraka kufika katika makazi yao.

Mkurugenzi wa Maendeleo na Usafirishaji wa DART Bw. Victor Ndonne aliwaambia wananchi hao kuwa amefurahishwa na hatua ya busara na utu waliyofikia ya kukubali ujenzi huo uanze kwani una manufaa katika maisha yao na vizazi vijanyo.

“Nimefurahi na kufarijika sana kuona kuwa sasa tumefikia makubaliano na wananchi waliokuwa bado hawajaridhia wameridhia ili kupisha ujenzi wa miundombinu hiyo.” Alisema Bw. Ndonne.

Bwana Ndonne aliongeza kuwa Serikali yetu ni Serikali inayowajali na kuwasikiliza wananchi ndo maana nasi wataalam wa DART na Temeke tumekuwa mara kwa mara tukifanya vikao na wananchi wa

Mbagala ili kila mmoja aridhike na hatimaye ulipwaji wa fidia ufuate kadiri ya kanuni na taratibu za ulipaji zilizopangwa,

Kwa upande wake Bw. Farid Salum ambaye ni mmiliki wa Simba Oil na mmojawapo aliyeridhika na maelezo ya wataalam yaliyotolewa kwake juu ya ulipwaji wa fidia katika eneo lake, aliwashukuru sana wataalam hao na kukubaliana na ujenzi huo.

“Nimeridhika na maelezo ya wataalam wa DART na Temeke ambayo hapo awali bado nilikuwa katika njia panda za ulipwaji wa fidia hizo na sasa nakubaliana na wananchi wenzangu ambao tayari waliridhia ujenzi huo uanze kwa vile ni wa manufaa kwa wananchi wa Mbagala na vizazi vijavyo.” Alisema.

Suala la vikao na wananchi wa Mbagala ili kupisha ujenzi wa Miundombinu ya DART lilianza toka mwaka jana mwanzoni 2017 na sasa hatua ya ulipwaji fidia imefikia hatua za mwisho na mara baada ya ulipwaji wa fidia hizo ujenzi huo utaanza.

-Mwisho-

Tanzania Census 2022