Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART yakutana na wadau kuweka sawa ujenzi wa BRT Awamu ya Tano barabara ya Mandela
17 Mar, 2026
DART yakutana na wadau kuweka sawa ujenzi wa BRT Awamu ya Tano barabara ya Mandela

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umepiga hatua nyingine muhimu kuelekea kuanza kwa ujenzi wa miundombinu ya mradi wa BRT Awamu ya Tano, utakaopita katika Barabara ya Mandela.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kikao kazi kilichofanyika leo, Machi 17, 2026, kikihusisha wadau wa sekta ya usafirishaji, biashara, na viongozi wa maeneo husika.

Kikao hicho kililenga kuweka misingi ya ushirikiano na uelewa wa pamoja ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi bila kuwepo kwa vikwazo vya kijamii au kiufundi.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, CPA Adv. Jerome Pantaleo Rweshagara, alisisitiza kuwa utoaji wa elimu kwa wadau ni nguzo kuu ya mafanikio ya mradi huu:

"Utoaji wa elimu kwa wadau ni hatua muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja, kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji, na kuhakikisha wananchi pamoja na taasisi zinazohusika wanashiriki kikamilifu katika kufanikisha mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam."

CPA Jerome aliongeza kuwa, licha ya kuwa kipindi cha ujenzi kinaweza kuleta mabadiliko ya muda mfupi katika mzunguko wa magari, ushirikishwaji huo utasaidia mradi kukamilika kwa wakati na kutoa huduma inayozingatia hadhi ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndg. Elihuruma Mabelya, alibainisha kuwa Awamu ya Tano ni mkombozi wa msongamano katika Barabara ya Mandela, ambayo ni kiungo muhimu cha kiuchumi

"Kupitia mchoro wa mradi huu, magari yatatengewa njia maalum, jambo litakalorahisisha mtiririko wa vyombo vya usafiri na kuongeza ufanisi wa kibiashara," alisema Ndg. Mabelya.

Naye Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa BRT kutoka TANROADS, Eng. Frank Mbilinyi, amewashukuru wadau kwa kujitokeza, akibainisha kuwa uelewa walioupata utasaidia kuondoa vikwazo vya miundombinu wakati mkandarasi atakapoingia kazini.

Mradi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi, ukidhihirisha imani ya washirika wa maendeleo katika maboresho ya miundombinu nchini Tanzania chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.Ujenzi wa mradi huu  unafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).