Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Ujumbe wa Benki ya Dunia wapongeza mfumo wa ukusanyaji nauli wa AFCS
19 Oct, 2023
Ujumbe wa Benki ya Dunia wapongeza mfumo wa ukusanyaji nauli wa AFCS

Benki ya Dunia imeupongeza Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwa kuwa na Mfumo bora na makini wa ukusanyaji wa nauli katika Mradi wa DART ujulikanao kama Automated Fair Collection System (AFCS).

Pongezi hizo zimetolewa na Ujumbe wa Benki ya Dunia (WB) ukiongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Wendy Hughes wakati wa ziara ya wajumbe hao walipotembelea miundombinu ya mradi Oktoba 19,2023.

Wakiwa katika Kituo cha Magomeni Kanisani na Kitengo cha TEHAMA cha DART cha Gerezani, ujumbe huo ulipata fursa ya kufahamu zaidi jinsi mfumo huo unavyofanya kazi ikiwemo udhibiti na ukusanyaji nauli ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za kila siku za kiutendaji zinazofanyika katika Mradi wa DART.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wa DART, Bw. Ngw’anashigi Gagaga akifafanua ujio wa wageni alisema “Si unajua ya kwamba kuona ni kuiamini, waliona ni vizuri kuona yale waliyokuwa wakiona kwenye maandishi na wamejionea kuanzia ukataji wa tiketi pale kwenye Piloti Kituo cha Magomeni Kanisani na kwenye uwasilishaji wa taarifa mbalimbali, wameshukuru na wanasema tuendelee, kazi ni nzuri “

Kuhusu hatua zinazoendelea za uandaaji wa Kadi janja, Gagaga amesema hatua iliyofikiwa ni nzuri na inaleta matumaini, kwani kadi zipo tayari na mageti yapo kwenye tathmini.

Aidha, Bw. Gagaga ametoa rai kwa abiria wanaosubiri Kadi Janja kuwa wakae mkao wa kula na wajiandae kutumia Kadi hizo kwani Wakala unafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa ili kadi hizo zianze kutumika rasmi.

Benki ya Dunia imefadhili ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka kwa Awamu ya Kwanza inayoendelea na huduma Kutoka Kimara na Matawi yake na Awamu ya Tatu kuelekea Gongolamboto na ile ya Awamu ya Nne kuelekea Tegeta ujenzi wake ukiendelea.