News

Watumishi wapya BRT wapewa mafunzo ya Usalama na Uokozi


Watumishi wapya BRT wapewa mafunzo ya Usalama na Uokozi

Watumishi zaidi ya 100 ambao ni waajiriwa wapya katika mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka DART wamepatiwa mafunzo maalum ya utayari wa kupambana na maafa uokoaji pamoja na huduma ya kwanza ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa DART wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam, Mhandisi Ahmed Wamala alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kutoa msaada na uokoaji pale ambapo yatatokea maafa ama ajali katika mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu na ni mwendelezo wa maono na falsafa ya Mtendaji Mkuu Dkt.Edwin Mhede ya kufanya usafirishaji wa umma katika Jiji la Dar es Salaam uwe wa kuaminika na salama zaidi wakati wote, hivyo kuendelea kujenga kuaminika zaidi kwa watumiaji wa huduma zetu” Alisema.

Aidha Mhandisi Wamala alisema huduma ambayo haina usalama wa kutosha na ambayo haimhakikishii usalama mteja katika kipindi hiki cha ushindani kibiashara haina nafasi hivyo akawaasa washiriki kuwa makini na kujifunza mbinu zote za uokozi na huduma ya kwanza kwaajili ya kusaidia pale ambapo maafa na ajali zitatokea.

Kwa upande wake Mkufunzi na Mtaalam wa masuala ya uokozi huduma ya na utayari katika kukabiliana na maafa Dkt. Amini Mshana alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa watumishi kwaajili ya kuboresha na kuimarisha utendaji wao wa kazi, lakini pia hata kwaajili ya faida binafsi kwani wataweza kutoa usaidizi mahala popote patakapotokea majanga kama ajali, moto nakadhalika.

“Naipongeza menejimenti ya Wakala kwa kuona umuhimu wa kuwapatia mafunzo wafanyakazi wapya ambao wamejiunga kufanya kazi katika mfumo, hii itawajengea wateja Imani ya kwamba wanahudumiwa na watu makini ambao hata yakitokea maafa ama ajali wataweza kutoa usaidizi wa haraka na hata kuwaokoa”Alisema.

Miongoni mwa mada zilizotolewa ni pamoja na utayari wa kupambana na majanga hasa ajali za mabasi, moto, mafuriko pamoja na jinsi ya kuhudumia mtu aliyezimia, mtu aliyepata mshituko wa moyo, mtu anayetoka damu kwa wingi pamoja na hatua muhimu za awali za kufanya mara ajali inapotokea.

Watumishi waliopatiwa mafunzo hayo ni pamoja na madereva wapya 47 askari wa kampuni ya ulinzi ya China Tanzania 48 pamoja na watumishi wengine 15 kutoka Kampuni ya mtoa huduma ya Mabasi UDART pamoja na DART.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa jitihada za Mtendaji Mkuu wa DART Dkt.Edwin Mhede kuwajengea uwezo watumishi wanaofanya kazi katika mradi ili waweze kutoa huduma bora na kuongeza tija, na ni katika kupanua wigo wa kueneza falsafa ya KAIZEN ambayo inaongeza uwajibikaji, tija na kuleta maboresho chanya katika utendaji kazi.