News

​Waziri Bashungwa ampa kongole Dkt.Mhede kwa kuvuka lengo ukusanyaji mapato.


Waziri Bashungwa ampa kongole Dkt.Mhede kwa kuvuka lengo ukusanyaji mapato.

Na. Mwandishi Wetu.

WAZIRI wa Nchi Ofisi Rais Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka(DART) Dk.Edwin Mhede kwa kubuni mikakati ya ukusanyaji mapato pamoja na kuwafichua wale wote wanaohusika na upotevu wa mapato, jambo ambalo limeuwwezesha Wakala huo kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia 120.

Akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART, alipofanya ziara ya kuona maendeleo ya mradi huo Jijini Dar es Salaam, Wazizi Bashungwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya uamuzi sahihi na wa kupongezwa kwa kumteua Dkt.Mhede kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo.

“ Nichukue fursa hii kipekee kabisa kumshukuru Mh.Rais kwa kukuleta hapa, wewe ni mtu sahihi kabisa maana kabla yako mambo yalikua hayaendi lakini sasa umeonyesha kwamba miradi mikubwa ya serikali nay a kimkakati kama huu ikisimamiwa vizuri inaweza kuleta tija kwa wananchi ambao ndio tumeaminiwa kuwatumikia” Alisema Waziri Bashungwa.

Wazizi Bashungwa aliitaka DART kutobweteka na mafanikio hayo na kuongeza juhudu, maarifa na ubunifu ili waweze kuvuka lengo kwa asilimia nyingi zaidi na hatimaye waongeze wigo wa utoaji huduma na kutatua kabisa changamoto ya usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam.

Aidha Waziri Bashungwa alisema, Serikali itaendelea kusimamia na kuusaidiw Wakala huo ili uweze kuongeza wigo wa upatikanaji wa usafiri wa haraka na wa uhakika katika maeneo mengine ya Jiji lakini pia hata nje ya Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kwa sasa mkoa wa Pwani umeshaunganika na Dar es Salaam na unahitaji usafiri wa uhakika.

“Zamani mkoa wa Pwani na Dar es Salaam ilionekana kuwa ni maeneo ambayo yako mbali sana, lakini kutokana na maendeleo sasahivi mikoa hii imeunganika hivyo tujitahidi katika mipango yetu tufungue njia za usafiri kuunganisha mikoa hii na jambo hili litasaidia kukuza uchumi kwani mkoa wa Pwani ni mkoa wa kimkakati wa Viwanda” Alisema.

Waziri Bashungwa pia, aliagiza Wakala kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuboresha huduma sambamba na kuboresha huduma kwa kushirikisha sekta binafsi kwani miradi mikubwa ya namna ya DART duniani kote inaendeshwa kwa ufanisi kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dkt.Edwin Mhede, alimweleza Waziri kuwa Wakala katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 umepanga kutumia Sh. Bilioni 7.02 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vyake ambapo kati ya fedha hizo Sh. Bilioni 6.72 ni matumizi ya kawaida na Sh. Milioni 298 ni kwa ajili ya ukarabati wa kawaida wa miundombinu ya awamu ya kwanza.

Alisema katika fedha hizo kiasi cha Sh. Bilioni 7.02, Sh Bilioni 2.25 ni ruzuku kutoka Serikalini Sh. Bilioni 4.76 ni mapato ya ndani huku katika kipindi cha Julai hadi Desemba wakala ukikusanya kiasi cha Sh. Bilioni 4.5 sawa na asilimia 128.43 ya malengo ya kukusanya Sh Bilioni 3.5.

Dkt.Mhede alisema Wakala unaendelea na kazi ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya pili kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi tatu ambapo hadi kufikia mwezi Desemba mwaka jana ujenzi wake ulikua umefika asilimia 44.4 na matarajio ni kwamba ikiwezekana ifikapo mwezi Machi,2023 mradi utazinduliwa na kuanza kutoa huduma.

Mtendaji Mkuu pia alimwambia Waziri kuwa, Wakala unaendelea na mkakati wa muda mfupi wa kuongeza mabasi 95 na hivyo kufikisha idadi ya mabasi 305 yanayohitajika kutoa huduma katika Awamu ya kwanza ya mradi.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt.Grace Magembe alisema kwakuwa mradi wa DART ni wa kimkakati na lengo lake ni kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi watahakikisha wanausaidia Wakala ili kuweza kusimamamia ipasavyo mradi huo ambao ni kioo kwa nchi ikizingatiwa watu wengi kutoka mataifa mbali mbali wanakuja kujifunza.

Mwisho.