Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Zabuni ya Usimikaji wa Mfumo Nadhifu wa Kuongozea magari (ITS) yafunguliwa
13 Nov, 2025
Zabuni ya Usimikaji wa Mfumo Nadhifu wa Kuongozea magari (ITS) yafunguliwa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka - DART leo  November 13, 2025 umefanya ufunguzi wa zabuni ya Mfumo Nadhifu wa Kuongozea Magari ‘Intelligence Transportation System (ITS)’ iliyotangazwa mwezi Machi 2025.

Ufunguzi wa zabuni ulifanyika mbele ya Wazabuni waliowasilisha maombi ya kumpata Mkandarasi atakae pewa jukumu la kutengeneza na kusimika Mfumo huo nadhifu wa kuongezea magari.

Akizungumza baada ya ufunguzi huo Mwenyekiti wa Kamati ya Ufunguzi wa Zabuni Bw. Joseph Charos ameeleza kuwa awali walijitokeza waombaji 18 na baada ya mchujo wa awali wakasalia waombaji sita.

“Awali walijitokeza waombaji 18 na baada ya mchujo wa awali wakasalia waombaji sita ambao hadi kufikia mwisho wa kuwasilisha maombi ya zabuni ni Kampuni tano pekee ndizo zilizowasilisha maombi.” alisema Charos.

Bw. Charos alizitaja Kampuni hizo kuwa ni Twende Consortium kutoka Afrika Kusini, SICE Sociedad Iberica De Construcciones Electricas ya Hispania, Derm Group Tanzania Ltd kutoka Tanzania, Shenzhen I.T.S Technology Co.Ltd, JV of Shandong High Speed Information Group Co.Ltd and Zhengzhou Tiamaes Technology Co.Ltd kutoka nchini China.

Aidha Bw. Charos alisema, katika Kampuni sita zilizopatikana baada ya mchujo, ni Kampuni ya AVIC pekee ndiyo haikuweza kuwasilisha maombi.

Hata hivyo Bw. Charos aliongeza kuwa DART kwa kushirikiana na Kampuni ya IDOM kutoka Hispania ambaye ndiye Mhandisi Mshauri, watafanya mapitio na uchambuzi wa maombi hayo ndani ya mwezi mmoja ili kumpata mzabuni aliyeshinda.

Kazi ya usimikaji wa Mfumo Nadhifu wa Kuongozea Magari utakaohusisha Uwekaji wa Taa za Barabarani, Kamera za Usalama pamoja na mambo mengine, unafadhiliwa na Benki ya Dunia na pindi utakapokamilika utasaidia kudhibiti na kutoa taarifa zitakazoongeza ufanisi wa mwenendo wa mabasi.

Vilevile Mfumo huo wa ITS utasaidia kuondoa changamoto ya uchelewaji wa magari kwenye makutano ya barabara za mabasi Yaendayo Haraka na magari mengine na pia utasaidia kufahamu idadi ya mabasi yanayohitajika na usalama wa abiria na mali zao wakiwa kwenye safari ndani ya Mfumo wa DART.