HOTUBA YA MTENDAJI MKUU WA WAKALA WA MABASI YAENDAYO HARAKA-DART, DR. EDWIN P. MHEDE WAKATI WA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KATIKA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI TAWI LA MLOGANZILA TAREHE 8 MACHI 2022

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,

Mkurugenzi Tawi la Mloganzila,

Menejimenti na Wafanyakazi Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mloganzila,

Watumishi wa DART,

Waandishi wa Habari,

Wakazi wote wa Kibamba na maeneo ya Jirani na Hospitali,

Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha sisi sote kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Pia nichukue fursa hii kuwapa pole wagonjwa na wale wanaopitia changamoto mbali mbali za kiafya, nawaombea mpone haraka ili mkashiriki katika kazi za kulijenga taifa letu.

Kipekee, nichukue fursa hii kuushukuru Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Upanga na hapa Mloganzila, kwa kutukubalia kuja kutembelea wagonjwa katika siku hii muhimu ya Wanawake Duniani ili kuwafariji pamoja na kutoa zawadi mbalimbali kama mchango wa taasisi kwa jamii.

Aidha, nichukue fursa hii pia, kuwashukuru watumishi wote wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ambao wameambatana nami kuja kuonyesha upendo wetu kwa wenzetu hapa Mloganzila; nimefarijika kwa kuwa tumeshirikiana wote bila kujali wanaume wala wanawake ingawa leo ni siku ya Wanawake Duniani.

Ndugu Viongozi na wote mlioko hapa, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka-DART kama zilivyo Taasisi nyingine za serikali, tunatekeleza kwa vitendo falsafa na maono ya Mama yetu mpendwa Mh. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya kazi kwa bidii huku tukijali afya za wengine kwani afya bora ndio mtaji wa kufanya kazi kwa ufanisi; hivyo tumemuunga mkono kwa kuja kuleta vitu vichache ambavyo vitasaidia wenzetu wagonjwa katika Hospitali hii.

Ndugu Zangu, Falsafa ya Mh. Rais na Kauli Mbiu yake ya KAZI IENDELEE itakuwa na maana zaidi kama itaungwa mkono na wadau kutoka katika sekta mbalimbali ili hatimaye Tanzania yenye afya bora na maendeleo iweze kupatikana na ionekane duniani kote kama ambavyo Mh.Rais ameendelea kuitangaza ramani ya nchi yetu huko nje kwenye ziara za hivi karibuni ambazo zimezaa matunda mengi na zimeleta tija katika sekta mbali- mbali ikiwemi hii ya kwetu ya usafiri wa umma.

Ndugu Zangu, Katika kuendelea kutoa huduma bora za usafiri hapa Dar es Salaam Wakala umeanzisha safari za Mabasi Yaendayo Haraka kutoka Kimara kuja hapa katika Hospitali ya Mloganzila; hii ni katika kuitikia kilio cha muda mrefu cha wananchi cha kupatiwa usafiri wa haraka na wa uhakika, pia kusogeza huduma kwa wananchi hasa wale wenye mahitaji maalum wakiwemo wagonjwa, wajawazito, walemavu pamoja na wazee ambao usafiri usiokuwa rafiki unawaathiri sana kutokana na hali zao.

Tumeamua kuleta Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka hapa Mloganzila japo miundombinu hairuhusu kama vile barabara maalum za mabasi, vituo kwa ajili ya kusubiria na kupumzikia abiria pamoja na sehemu mahsusi kwa ajili ya kukatia tiketi na hata huduma ya choo, haya yote ni mapenzi tuliyo nayo kwa Watanzania wenzetu ambao tunawahudumia kila siku.

Ndugu Zangu, katika kuiadhimisha siku hii ya Wanawake Duniani, tuliona ni vyema kama taasisi tuchangie walau kiasi kidogo tulichojaaliwa ili kiwasaidie na wenzetu wagonjwa na wenye mahitaji mbali mbali hapa Mloganzila ikiwa ni sehemu ya mchango wetu katika jamii tunapotolea huduma ya usafiri wa umma.

Kutokana na umuhimu wa siku yenyewe, Wakala umeleta Mashuka, Diapers, Sabuni, Mafuta ya Nazi, dawa za meno, pads, ndala, mashine ya kupimia presha pamoja na kiti cha magurudumu (Wheel chair) kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa.

Tunawaomba mpokee hicho kidogo tulichowaletea ili kiweze kusaidia kupunguza changamoto kwa wagonjwa; huu ni mwanzo tu huko mbele kadiri tutakavyokua tunaendelea kutoa huduma, tutaendelea pia kujitoa kwa wenzetu kwani kutoa ni moyo wala sio utajiri.

Ndugu Zangu, kwa kumalizia, nichukue fursa hii kuwashukuru wote waliofanikisha tukio hili la leo, na niwahakikishie kuwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART utaendelea kuboresha huduma zake ili kupunguza kero ya usafiri wa umma kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Jirani.

Asanteni sana kwa kunisikiliza na sasa niko tayari kukabidhi vile nilivyokuja navyo.

Mwisho.