Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART yaongeza kasi kurejesha huduma ya mabasi baada ya ghasia za uchaguzi
21 Nov, 2025
DART yaongeza kasi kurejesha huduma ya mabasi baada ya ghasia za uchaguzi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imeongeza kasi ya juhudi za kurejesha huduma za BRT kufuatia uharibifu wa miundombinu uliotokana na ghasia ya tarehe 29 Oktoba 2025. Kwa mujibu wa DART, tathmini ya kina imekamilika na sasa hatua za ukarabati zinaendelea kwa kasi ili kurejesha huduma kwa awamu.

DART imeeleza kuwa Awamu ya Kwanza ndiyo iliyoathirika zaidi, ikiwa na uharibifu mkubwa katika vituo, na barabara maalum za mwendokasi, mifumo ya umeme na vifaa vya TEHAMA. Baadhi ya vituo vimeungua, vioo kuvunjika, mifumo ya kukusanyia nauli kung’olewa, vibanda vya tiketi kuharibika, na mifumo ya matangazo na ulinzi kuathirika.

Aidha, vituo vya njia mlishi kati ya Kimara na Kibamba vimepata athari kubwa, ambapo vibanda vingi vya tiketi vimeungua kabisa, jambo lililosababisha kusimamishwa kwa muda kwa huduma za utoaji tiketi katika maeneo hayo.

Kwa upande mwingine, Awamu ya Pili—katika Barabara ya Kilwa iendayo Mbagala—imepata uharibifu mdogo ukilinganishwa na Awamu ya Kwanza. Baadhi ya vituo vimepata uharibifu wa vioo, na vyumba vya tiketi, lakini miundombinu mikubwa imebaki imara.

Kutokana na kiwango cha uharibifu, DART imethibitisha kuwa Awamu ya Kwanza inahitaji ukarabati mkubwa kabla ya kurejeshwa kwa huduma, huku Awamu ya Pili ikiwa tayari kuanza kutoa huduma tarehe 20 Novemba wakati marekebisho yakikamilishwa.

Timu maalum za ukarabati zimeanza kazi katika maeneo yaliyoathirika zaidi ya Awamu ya Kwanza, zikijikita kurejesha miundombinu, mifumo ya umeme na TEHAMA ambayo ni muhimu katika uendeshaji wa huduma.

Wakala pia umetangaza kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo yote ya mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka, iakiwemo vituo vikubwa, na barabara maalum, ili kuzuia uharibifu zaidi na kulinda mali za umma wakati wa ukarabati.

DART imesisitiza kuwa kutoa taarifa kwa wananchi ni kipaumbele, na kwamba taarifa za mara kwa mara zitatolewa kuhusu maendeleo ya ukarabati na hatua za kurejesha huduma.

Kwa mujibu wa DART, huduma za sehemu katika Awamu ya Pili zinatarajiwa kurejea hapo tarehe 20 Novemba, ambapo vituo vya Zakhem na Mbagala Rangi Tatu vitatoa huduma kwa kiwango kidogo wakati ukarabati ukiendelea.

Wakala umeeleza kuwa kurejesha mfumo wa mwendokasi ni muhimu kwa kuhakikisha usafiri wa uhakika na salama kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam. DART imerejea dhamira yake ya kufanya shughuli za ukarabati kwa kasi na uwazi.

Mara ukarabati utakapo kamilika, Serikali inalenga kurejesha mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka kikamilifu na kujenga upya imani ya wananchi katika mfumo huu muhimu wa usafiri wa umma.