Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Wanawake wa DART Waadhimisha Siku ya Wanawake kwa Vitendo: Waelekea Gereza la Segerea
06 Mar, 2026
Wanawake wa DART Waadhimisha Siku ya Wanawake kwa Vitendo: Waelekea Gereza la Segerea

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) wameamua kuifanya siku hii kuwa ya kipekee kwa kugusa maisha ya wengine.

Wakiongozwa na moyo wa upendo na mshikamano, wanawake hao wameelekea katika Gereza la Segerea kutoa msaada kwa wafungwa wanawake na watoto walio gerezani hapo.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: "Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi jumuishi kufikia Dira 2050."

Kauli mbiu hiyo yenye ujumbe wa Matumaini na Ujumuishi, kwa wao wanaona safari hii ya kutoa msaada ni kielelezo tosha kuwa kufikia Dira ya 2050, hakuna mwanamke anayepaswa kuachwa nyuma, bila kujali mazingira aliyopo.

Wanawake wa DART wamebainisha kuwa haki na usawa huanza na kutambua utu wa kila mwanamke na kumpa msaada wa kisaikolojia na mahitaji muhimu ili kumjengea msingi wa kurejea kwenye jamii kwa tija.

"Tunaelekea Gereza la Segerea kuonyesha kuwa tunawajali dada zetu na ndugu zetu. Usawa tunaoupigania ni ule unaovuka kuta za ofisi zetu na kufika hadi kwa wale walio pembezoni," alisema Mwamvua Stambuli ambaye ni Mwenyekiti wa wafanyakazi wanawake DART.