DART yawahakikishia abiria huduma ya usafiri wakati wa El Nino, daraja la Kigogo na Mkwajuni kuwa njia mbadala kwa Jangwani
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umewahakikishia wananchi kuwa huduma za usafiri wa mabasi ya mwendokasi kuelekea katikati ya jiji hazitasimama wakati wa msimu wa mvua za El Nino, kutokana na kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kupitisha mabasi kupitia madaraja ya Kigogo Sambusa na Mkwajuni.
Akizungumza wakati wa kupokea gari jipya la dharura la kunyonya maji taka leo Septemba 12, 2026, Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Saidi Tunda, amesema madaraja hayo mawili yatatumika kama njia mbadala za kupitishia mabasi yanayotokea Kimara kuelekea mjini endapo eneo la Jangwani litajaa maji wakati huu ujenzi wa daraja ukiendelea.
Bw. Tunda ameeleza kuwa hatua hii inalenga kuondoa adha kwa abiria wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Kwanza ambao hutegemea usafiri huo kila siku, huku akisisitiza kuwa wakala umejipanga kikamilifu kuhakikisha miundombinu inabaki salama na inafanya kazi bila kukwama.
"Tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata huduma ya usafiri bila kukwama hata pindi mvua kubwa za El Nino zinaponyesha na kusababisha mafuriko Jangwani. Mabasi yetu yatatumia njia mbadala kupitia madaraja ya Kigogo Sambusa na Mkwajuni ili safari za kuelekea mjini zisiweze kusimama," alieleza Bw. Tunda.
Njia hizi mbadala zinaongeza nguvu kwenye juhudi za DART za kukabiliana na athari za mvua, sambamba na kupokelewa kwa gari hilo la dharura litakalosaidia kuondoa maji yatakayotuama katika maeneo yasiyostahili kwenye barabara na vituo vya BRT.
Gari hilo limekabidhiwa kwa DART kutoka Kampuni ya M/s Mohammedi Builders ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Awamu ya Kwanza, uliogharamiwa na Benki ya Dunia.
