Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DART yajiimarisha dhidi ya El Nino, yakabidhiwa gari jipya la dharura kulinda miundombinu ya BRT
12 Sep, 2026
DART yajiimarisha dhidi ya El Nino, yakabidhiwa gari jipya la dharura kulinda miundombinu ya BRT

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umechukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto za mafuriko na maji yaliyotuama wakati wa msimu wa mvua, baada ya kupokea gari maalum la kisasa la kunyonya maji taka litakalotumika pia kama ngao ya dharura kwenye miundombinu ya usafiri huo.

Gari hilo limekabidhiwa kwa Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Saidi Tunda, leo Septemba 12, 2026, na Kampuni ya M/s Mohammedi Builders.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya mabasi yaendayo haraka Awamu ya Kwanza, uliogharamiwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa Output and Performance Based Contract for the Maintenance of the BRT Infrastructure (OPBC) - Phase 1.

Akizungumza mara baada ya kupokea gari hilo, Bw. Tunda amesisitiza kuwa ujio wake umekuja wakati muafaka ambapo wakala huo unajipanga kikamilifu kukabili athari za mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwisho wa mwezi huu wa Septemba 2026.

Bw. Tunda ameeleza kuwa mbali na kazi yake ya kawaida ya kuondoa maji taka katika maliwato za vituo vya BRT, gari hilo limepewa jukumu la kimkakati la kutoa maji yatakayotuama katika maeneo yasiyostahili kwenye miundombinu ya DART—kama vile barabara za mabasi yaendayo haraka na ndani ya vituo ili kuhakikisha huduma ya usafiri inaendelea hata wakati wa mvua kubwa.

"Gari hili litakuwa msaada mkubwa sana. Lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kupata huduma ya usafiri bila kukwama pindi barabara zetu zinapofurika maji au kwenye vituo wakati wa mvua za El Nino,” alisema Bw. Tunda. “Litafanya kazi ya kunyonya na kuondoa maji hayo kwa haraka ili wananchi waendelee kupata huduma ya usafiri kama kawaida."

Mapokezi ya gari hili la dharura yanakuja sambamba na kukamilika kwa kazi ya ukarabati wa vituo 14 vya Mabasi Yaendayo Haraka iliyotekelezwa chini ya mradi wa OPBC.

Vituo vilivyofikiwa na ukarabati huo ni pamoja na Kimara, Korogwe, Bucha, Baruti, Corner, Kibo, Ubungo Maji, Ubungo Terminal, Shekilango Feeder, Urafiki, Tiptop, Manzese, na Argentina.

Aidha,ukarabati huo uliofanyika ulihusisha kuboresha mifumo ya umeme, kuweka mifumo ya nishati jua katika kituo cha Kimara, Korogwe, Manzese, na Msimbazi B kama nishati mbadala wakati wa kukatika kwa umeme, pamoja na kufanya ukarabati wa majengo ikiwemo paa, milango, kupaka rangi, uwekaji marumaru, na vyoo.

Kupitia hatua hii, DART inaonyesha utayari wake wa kiutendaji katika kulinda miundombinu ya mradi huo, huku ikihakikisha abiria wa Jiji la Dar es Salaam wanasafiri kwa usalama, ufanisi, na bila kukwama nyakati zote.