DART yaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kupima afya za Abiria bure
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kwa kushirikiana na watoa huduma wake Kampuni ya UDART na Mofat, wameendesha zoezi maalumu la upimaji wa afya kwa abiria wanaotumia usafiri huo. Hatua hii ni sehemu ya mkakati kabambe wa kuhakikisha abiria wanapata thamani halisi ya huduma wanazozilipia.
Zoezi hilo la huduma ya afya bure lilifanyika kuanzia tarehe 05 hadi 09 Oktoba 2026 katika vituo vikuu vya mabasi hayo. Lilianzia katika Kituo Kikuu cha Kimara, kuendelea katika vituo vya Gerezani (Awamu ya Kwanza na Pili) na Mbagala, kabla ya kuhitimishwa rasmi katika Kituo Kikuu cha Kivukoni. Katika vituo hivyo, wataalamu na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) walitoa huduma hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Kupitia zoezi hilo lililofanyika mahsusi kwa ajili ya wiki ya huduma kwa wateja, jumla ya abiria 981 walipima afya zao na kupongeza DART kwa ubunifu huo na utayari wa kuwaletea wataalamu wa afya karibu na maeneo yao ya usafiri.
“Mimi nawashukuru sana DART kwa kutuletea wataalamu hawa. Binafsi nilikuwa nikienda Kariakoo kwenye shughuli zangu, sasa nikaona nitumie fursa hii adimu kucheki afya yangu. Nimepima shinikizo la damu, sukari, na pia nimepata ushauri kuhusu lishe bora na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Adinani Kisandu, mkazi wa Kimara Bonyokwa.
Kwa upande wake, Tamimu Mohammed, aliyepata huduma katika Kituo Kikuu cha Gerezani (upande wa Mbagala), alieleza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa abiria kupatiwa huduma za upimaji wa mara kwa mara kwa kuwa wengi wao hukosa muda wa kwenda hospitalini kutokana na ratiba zao ngumu.
“Ndugu yangu, haya mambo mngekuwa mnayafanya mara kwa mara mngetusaidia sana. Kwa mfano, mimi kulingana na shughuli zangu, natoka mapema sana nyumbani na nachelewa kurudi; hivyo upimaji huu hapa vituoni umenisaidia sana,” alisema Bw. Tamimu.
Akihitimisha zoezi hilo, Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Said Tunda, aliwashukuru abiria wote kwa kuendelea kuwaamini na kutumia huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka, akiwahakikishia dhamira ya wakala ya kuendelea kuboresha huduma ili kukidhi matarajio yao.
“Napenda kuwashukuru abiria wote kwa kuendelea kutuamini na kutumia huduma zetu. Tunapohitimisha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja kwa mwaka huu 2026, tunawahakikishia kuwa dhamira yetu ni kuendelea kuboresha huduma zetu ili zikidhi na kuwapa kile wanachokitazamia,” alisema Bw. Tunda.
Aidha, Mtendaji Mkuu aliwasihi abiria kutofumbia macho changamoto zinapojitokeza, na endapo wana maoni au mapendekezo, wawasiliane na wakala kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 0800110147 au kupitia barua pepe mteja@dart.go.tz.
Zoezi hilo la upimaji afya katika vituo vikuu lililenga kuwapunguzia abiria usumbufu wa safari za kwenda hospitalini, sambamba na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kutambua dalili na viashiria vya magonjwa mapema ili kuchukua hatua stahiki za matibabu na kujikinga.
