News

​DART Taasisi ya Kwanza sekta ya Usafirishaji Kutekeleza KAIZEN.


Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART imekua taasisi ya kwanza ya serikali inayojihusisha na masuala ya usafirishaji kutekeleza falsafa ya kuleta mabadiliko chanya katika kuleta maendeleo na tija, KAIZEN.

Akizungumza Mjini Kibaha mwishoni mwa wiki katika kikao cha kuhitimisha wiki saba za mafunzo ya KAIZEN kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka , Mtendaji Mkuu wa DART Dkt.Edwin Mhede amesema taasisi yake kuwa ya kwaza kutekeleza falsafa hiyo kwenye sekta ya usafiri wa umma ni juhudi zilizopo za kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii na kuwarahisishia maisha wananchi wa mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

“ Falsafa ya KAIZEN ni kitu kinachotumiwa na wenzetu wajapani na kimewawezesha kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo hasa katika masuala ya viwanda na biashara, kutokana na kufanikiwa huko falsafa hiyo imeenezwa hata katika sekta nyingine na inaonyesha matokeo mazuri hasa katika utoaji huduma kwa jamii pamoja na kuisaidia jamii na wafanyakazi kuwa na mabadiliko ya fikra katika utendaji kazi” Alisema Dkt.Mhede.

Alisema matumizi ya KAIZEN husaidia taasisi kuongeza ubunifu zaidi katika kutoa huduma zake ndio maana kwa sasa wameanzisha safari za Mabasi Yaendayo Haraka kunzia Kimara Hadi Kibaha mkoani pwani bila hata kukamilika kwa miundombinu ili kuwaletea wananchi ahueni ya usafiri wa umma.

“Kwakutumia ubunifu wa Kikaizeni tuliona sio vyema kuendelea kusubiria hadi miundombinu ya barabara maalum kwaajili ya Mabasi ikamilke, tumejiongeza na ndiomaana mtaona huduma inaendelea kama kawaida hapa Kibaha na wananchi wanaifurahia mno” Alisema.

Mtendaji Mkuu huyo wa DART, alisema sekta ya usafiri wa umma inatumiwa na watu wengi hasa mijini ndiomaana wameamua kuingiza fasafa ya KAIZEN katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wasafiri, lakini pia kuongeza ufanisi katika suala zima la kuhudumia wananchi.

Aidha Dkt.Mhede alisema kuwa, tafiti wanazofanya katika njia mbalimbali zitawawezesha kuanzisha safari za Mabasi Yaendayo Haraka mapema iwezekanavyo kabla ya ujenzi wa miundombinu ili kuwapunguzia kero ya usafiri wakazi wa maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

“Tunafikiaria pia kuanzisha safari za Mabasi yetu hadi vikindu ambapo pia ni sehemu ya mkoa wa Pwani, hii itasaidia wakazi wa maeneo ya jirani na wanaosafiri kutoka ama kwenda mikoa ya kusini kupata usafiri wa uhakika na wa haraka” Alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Jane Lyatuu, alisema kutekelezwa kwa falsafa hiyo kwa taasisi ya kwanza katika sekta ya Usafirishaji kuna amsha ari kwa taasisi nyingine za umma kuona umuhimu wa kuitumia ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza tija na ufanisi.

“Tumefurahi kuona DART imelichukua suala la matumizi ya KAIZEN kwa uzito mkubwa na kwa kipindi chote ambacho tumekua tukitoa mafunzo tumeona kuna mabadiliko makubwa sana ya utoaji wa huduma japo bado kuna baadhi ya changamoto” Alisema Bi. Lyatuu.

Alisema taasisi ambazo zinatumia falsafa ya KAIZEN zimefanikiwa sana kupunguza matumizi ya nafasi , muda, rasilimali na vifaa jambo ambalo linaokoa fedha na kuongeza ubunifu.

Mafunzo ya wiki saba juu ya falsafa ya KAIZEN kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ni moja ya mbinu za kuifanya taasisi iweze kuongeza kasi ya utoaji huduma bora kwa wananchi na yalijumuisha makundi mawili ya wataalam ambao ni machampioni ambao watatumika kueneza elimu juu ya falsafa hiyo kwa wafanyakazi wengine.

Mwisho.