Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Prof. Shemdoe azindua Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala, atoa maelekezo kuimarisha BRT
31 Jul, 2026
Prof. Shemdoe azindua Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala, atoa maelekezo kuimarisha BRT

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amezindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Wizara (MAB) ya DART na kuitaka itoe uongozi na ushauri utakaoharakisha maendeleo ya mradi wa BRT.

"Baada ya leo uteuzi umeisha. Kilichobaki ni matokeo ya kazi yenu. Baada ya miaka mitatu tujipime tumeongeza nini kwa DART," alisema Prof. Shemdoe.

Aliielekeza Bodi kutathmini mfumo bora wa uendeshaji, kuongeza vyanzo vya mapato, kuandaa DART kuwa mamlaka ya kitaifa, kufanya ziara za mafunzo na kupendekeza maboresho ya sheria na sera.

Pia aliagiza Bodi kuwa na mpango kazi wa kila robo mwaka na kupanga miundombinu ya muda mrefu.

Mwenyekiti wa Bodi, Bw. David Kafulila, aliishukuru Serikali kwa imani hiyo na kusema DART ni taasisi ya kimkakati.

"Tutafanya kazi bega kwa bega na Waziri na Menejimenti ya DART. Tutatoa ushauri wa kitaalamu na kupitia Mpango Mkakati," alisema Bw. Kafulila.

Alisema utaalamu wa wajumbe utasaidia kuimarisha maamuzi ya BRT.

Kwa niaba ya wajumbe, Dk. Nicous Herman Shombe alisema Bodi itafanya kazi sambamba na Waziri kuboresha usafiri wa umma Dar es Salaam.

"Tutashirikiana na Waziri na wadau wote kuhakikisha ushauri wetu unaleta maboresho ya kweli katika mfumo wa BRT," alisema Dk. Shombe.

Awali, Mtendaji Mkuu wa DART, Bw. Said Tunda, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi na mafanikio ya Wakala.

Alisisitiza kuwa Menejimenti ya DART itatekeleza ushauri wa Bodi kwa ufanisi.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa uzinduzi rasmi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara.