Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
DC Nyangasa Alilia Mwendokasi Kigamboni.
24 Apr, 2023
DC Nyangasa Alilia Mwendokasi Kigamboni.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Almasi Nyangasa ameuomba wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART kufikiria namna ya kupeleka huduma ya Mabasi kwa Wakazi wa Kigamboni kwani wana shida kubwa ya usafiri wa umma.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wan chi Ofisi ya Rais (Tamisemi) Angelah Kairuki alipotembekea DART katika kituo kikuu cha Kivukoni, Mkuu huyo wa Wilaya alisema wananchi wa Kigamboni wana kiu kubwa ya kuona huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka inafika Kigamboni kwani mji unazidi kukua kwa kasi na Wilaya hiyo mpya imeendelea kupata ongezeko kubwa la watu Pamoja na shughuli za kiuchumi kama viwanda na biashara.

“Mh. Waziri natambua kuwa DART katika mipango yao na awamu zao zote za mradi hakuna sehemu ambayo Kigamboni tutafikiwa na huduma hii, nikuombe kama itawezekana basi kupitia Daraja la Mwalimu Nyerere angalau wenzetu waone namna ya kuongeza wigo wa mtandao wa barabara zao ili na sisi wakazi wa kigamboni tuingie katika historia ya kupata huduma hii adhimu” Alisema DC Nyangasa.

 

Alisema katika siku za karibuni wananchi wa kigamboni waliona Mabasi Yaendayo Haraka ambayo yalikodishwa kwa shughuli maalum katika chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni wakampigia simu kuuliza maka sasa DART imeamua kupeleka huduma katika Wilaya yake.

 

Alisema alipofuatilia akagundua ni shughuli maalum tu ndio iliyofanya Mabasi Yaendayo Haraka kufika Kigamboni wala sio kwamba DART wameanza rasmi kutoa huduma katika wilaya hiyo.

 

Akijibu mapendekezo ya Mkuu huyo wa Wilaya Mtendaji Mkuu wa DART Dr.Edwin P.Mhede alisema kwakuwa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka umesanifiwa katika awamu sita ambazo kwa Kigamboni haufiki unaishia katika daraja la mwalimu Nyerere, watakaa na wataalam wa michoro ili kuona namna ambayo itafaa kuongeza wigo wa mtandao wa barabara za Mabasi Yaendayo Haraka ikiwemo kufika Kigamboni.

 

“Mimi ni raia wako Mh. DC kigamboni na mimi pia ni kwangu hivyo nitafanya kila mbinu kuona kama katika michoro na usanifu wetu tunaweza kupanua wigo ili kuwaletea huduma wakazi wa wilaya ya Kigamboni” Alisema Dr.Mhede.

Mtandao wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka ambao umesanifiwa kutekelezwa katika awamu sita unazihusisha wilaya zote za Dar es Salaam isipokua Kigamboni pekee, pia huduma za Mabasi mlishi zimeendelea kutolewa hadi maeneo ambayo hakuna barabara mahsusi kwa ajili ya Mabasi hayo kama Kibaha na Mloganzila.