News
Dkt. Mhede awataka watumishi DART kufanyakazi kwa umoja
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dkt.Edwin Mhede amewataka watendaji wa wakala kujituma na kufanya kazi kwa umoja kwani umoja ndio nguzo pekee ya mafanikio mahala pa kazi.
Dkt.Mhede ameyasema hayo Ijumaa tarehe 29 Aprili, 2022 katika Ofisi za Wakala Ubungo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa nasaha kwenye hafla ya kuwapongeza watumishi hodari waliochaguliwa kutoka katika Idara na vitengo mbalimbali.
“Nawapa siri ya mafanikio katika taasisi yoyote kufanya kazi kwa pamoja kunaleta tija na kunaongeza ufanisi, tofauti na taasisi ambayo kila mmoja anajiendea kivyake” Alisema Dkt.Mhede.
Alisema kuna usemi usemao kuwa famila moja hula pamoja hivyo kama tukitaka kuendelea kuwa pamoja kama timu tunatakiwa tufanye kazi kwa pamoja ndio maana ameona kuna umuhimu wa kuwa pamoja na wafanyakazi hodari ili kuwatia moyo kwa kutambua mchango wako katika taasisi.
Aidha alisema ni jukumu la kila mfanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa weledi kwani mamilioni ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanategemea kupata huduma bora ya usafiri wa haraka ambalo ndilo jukumu kubwa la wakala.
Katika hafla hiyo watumishi hodari kutoka katika idara za Utawala, Usimamizi wa miundombinu, Uendeshaji pamoja na vitengo vya Tehama, Ukaguzi wa ndani na Ugavi walipongezwa kwa utendaji wao.
Watumishi hao hodari waliopongezwa ni Bw. Bakari Mrope, Ezekiel Nyaisara, Geofrey Mgegwa, Deogratius Kilumile, Yahya Mgeni, Sila Okumu, Nebu Kyando na Bi. Adelphina Pweleza, ambaye ni mwanamke pekee katika wafanyakazi hao
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala Utumishi na Rasilimali watu Dkt. Eliphas Mollel alisema wazo la kuwapongeza watumishi hodari limetokana na maono ya Mtendaji Mkuu yafanya kitu cha utofauti ili kutambua mchango wa watumishi wanaojituma zaidi.
Alisema kutambua umuhimu wa mfanyakazi katika taasisi kunaongeza morali ya kufanya kazi hivyo zoezi hilo litakua endelevu na litaboreshwa ili kuongeza tija katika utendaji kazi wa kila siku wa Wakala.