Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka

"Usafiri wa Umma Nadhifu"

DART Logo
Kamati ya bunge yapongeza ujenzi wa awamu ya tatu
24 Mar, 2026
Kamati ya bunge yapongeza ujenzi wa awamu ya tatu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imepongeza maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu kando ya Barabara ya Nyerere iendayo Gongolamboto, ikisisitiza umuhimu wa kukamilika kwa wakati ili kuleta tija ya uwekezaji wa Serikali.

Kamati hiyo imetoa pongezi hizo Machi 23, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanyika chini ya uenyeji wa TANROADS, ambapo Wabunge wamepata fursa ya kuona maendeleo ya mradi huo moja kwa moja.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Japherson Michael Nnko, amewasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi wa BRT katika awamu zote sita, akielekeza zaidi katika Awamu ya Tatu.

Ameeleza kuwa Awamu ya Tatu yenye urefu wa kilomita 23.3 ni kiungo muhimu katika kuboresha usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na inaunga mkono mafanikio ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ambazo tayari zinafanya kazi.

Kamati imeridhishwa na maendeleo yanayoonekana na kubainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaonesha dhamira ya Serikali katika kuboresha huduma za usafiri wa umma.

Hata hivyo, Kamati imeielekeza TANROADS kuhakikisha inasimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza Awamu ya Tatu ili akamilishe ujenzi kwa wakati kama ilivyopangwa na kuleta tija ya uwekezaji uliowekwa na Serikali.

Aidha, Kamati imeelekeza kuwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) uandae mpango wa muda mrefu wa utekelezaji wa mradi huu unaofungamanishwa na Dira ya Taifa ya 2050 ili kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Kamati pia imesisitiza umuhimu wa kuunganisha miundombinu ya BRT na maeneo muhimu ya kushusha abiria kama vile kituo cha SGR, Uwanja wa Ndege na Bandari ili kuongeza ufanisi wa mfumo huo.

Vilevile, DART imetakiwa kuandaa mpango madhubuti wa ukarabati wa vituo vya BRT ili viendelee kuwa na ubora na ufanisi wa kutoa huduma.

Kamati imesisitiza usimamizi shirikishi wa mali za miradi ya BRT kwa kuwahusisha wadau muhimu kama TANROADS, TARURA, TRC, TAZAMA, TANESCO na wengine ili kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi.

Akijibu maswali ya Kamati, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Bw. Said Tunda, ameeleza namna mradi unavyosimamiwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Amefafanua kuwa Serikali imeweka nauli nafuu ili kuwahudumia wananchi, huku akibainisha kuwa faida za kiuchumi zinazotokana na mradi huo zitalipa kwa njia isiyo ya moja kwa moja gharama za uwekezaji.

Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameihakikishia Kamati kuwa Serikali itazingatia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa wakati.

Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu kutoka Office ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativira, viongozi na wataalamu kutoka DART na TANROADS pamoja na viongozi wengine wa Serikali, wakionesha mshikamano katika kufanikisha mradi huo.