PIC YATAKA MRADI YA BRT KULINDWA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu unaoanzia katikati ya Jiji hadi Gongo la Mboto ziara ambayo imeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh. Masanja Kadogosa kwa lengo la kujionea hatua zilizofikiwa katika mradi huo wa kimkakati.
Miradi ya Barabara za Mabasi Yaendayo Haraka BRTni sehemu ya mipango ya Serikali ya kupunguza msongamano wa magari na kero ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam ambayo inatekelezwa katika awami Sita.
Katika ziara hiyo Mhe Kadogosa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati nchini akibainisha kuwa utoaji wa fedha hizo kwa wakati ndio uliowezesha mradi huu wa awamu ya tatu kufikia hatua kubwa ya ukamilishaji ambapo kwa sasa ujenzi wa Vituo na Barabara za zege umeikia asilimia 99%.
Aliongeza kuwa, kuendelea kutolewa fedha za miradi ni Ushahidi kuwa Mheshimiwa Rais amedhamiria kupunguza ama kuondoa kabisa kero ya usafiri wa umma kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya Jirani, huku akieleza kuridhishwa kwake na kasi pamoja na ubora wa kazi inayofanyika kwa kuzingatia viwango vilivyopangwa.
Mwenyekiti huyo wa PIC pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wameutaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka -DART kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inalindwa ili iweze kutumika na kudumu kwa muda mrefu kama ilivyo lengo la Serikali kwa kujenga miundombinu hiyo.
Aidha, alisisitiza kuwa ni jukumu la Wakala kuwa na mikakati madhubuti ya kuzuia uharibifu wa miundombinu hiyo pamoja na wahujumu ili iweze kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka -DART Bwana Said Tunda amesema kuwa Wakala umepokea ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa na kamati na kwamba yatafanyiwa kazi kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija iliyokusudiwa.
