News
Saudia Yaonyesha nia kuwekeza kwenye Mwendokasi

Saudia Yaonyesha nia kuwekeza kwenye Mwendokasi
Na.Mwandishi Wetu.
Nchi ya Saudi Arabia imeonyesha nia ya kufanya uwekezaji mkubwa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) katika uendeshaji wa Mabasi, Teknolojia pamoja na mifumo ya uendeshaji kutokana na uzoefu wa miaka mingi walio nao katika sekta hiyo, lakini pia kutokana na Tanzania kuwa na mazingira mazuri na tulivu kwaajili ya uwekezaji.
Akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka pamoja na wawakilishi wa makampuni ya uwekezajikutoka Saudi Arabia,Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mh. Ally Mwadini amesema ujumbe huo umeonyesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya usafirishaji hasa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kutokana na mazingira wezeshi yaliyopo Tanzania ambayo yanawahakikishia wawekezaji uhuru wa kuwekeza.
“Leo tumekuja kwa ajili ya kuona ni namna gani Saudi Arabia inaweza kushiriki katika mradi huu wa Mabasi Yaendayo Haraka maarufu kama mwendokasi, hii inatokana nan chi ya Saudi Aarabia kuwa na uzoefu katika uendeshaji wa Miradi kama hii, lakini pia kwakua Tanzania ni nchi ya Amani na utulivu na yenye watu wakarimu pamoja na mazingiza wezeshi yaliyopo katika uwekezaji” Alisema Balozi Mwadini.
Amesema Tanzania ina umuhimu mkubwa sana kibiashara na uwekezaji katika ukanda huu wa Afrika kwani imepakana na nchi nyingi ambazo hutegemea huduma na bidhaa zake kupitia hapa nchini suala ambalo linawafanya wawekezaji kuona fursa hiyo na kuvutiwa kuja kuwekeza.
“Nimeambatana na wawakilishi wa kampuni ya Saudi Arabia Public Transport Company (SABTCO)pamoja na Taasisi ya Uwekezaji ambayo inahusika na kuwekeza nchini Saudi Arabia pamoja na nje ya nchi lengo kubwa ni kuja kuona na kutathmini namna watakavyoweza kuja kujiunga na Tanzania katika kuendeleza sekta ya Usafirishaji pamoja na sekta nyingine ambazo watavutiwa nazo” Alisema Balozi Mwadini.
Balozi Mwadini alisema Saudi Arabia ni nchi iliyoendelea na yenye mahusiano mazuri na Tanzania hivyo wameamua kuja kuunga mkono Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh.Samia Suluhu Hassan za kuwaletea Watanzania maendeleo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya SABTCO Bw.Hassan Abduljawad alisema wameona mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni eneo sahihi kwa wakati huu kutembelea na kuona namna wanavyoweza kuwekeza kwakua kuna awamu sita za mradi huo katika Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa watu wengi na wa fedha nyingi.
“Sisi tuna uzoefu wa kuendesha miradi kama hii kwa miaka mingi tumeona kwa awamu zote za mradi hapa Tanzania tunawez na sisi kuja kuwekeza katika moja ya awamu ili tuweze kutoa mchango wetu na uzoefu wetu kwa ajili ya watanzania” Alisema Bw. Abduljawad.
Ujio wa wawekezaji kutoka Saudi Arabia ni moja ya Juhuzi zilizotokana na ziara ya Mh.Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi za Ulaya na Falme za kiarabu za kutafuta wawekezaji kwaajili ya kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali hapa nchini.
Aidha kituo cha uwekezaji Tanzania TIC kimekua mstari wa mbele katika kutafsiri maono ya Rais Samia ya kutaka kuona Tanzania inayokua kiuchumi kupitia uwekezaji wenye tija kwa kuendelea kuratibu na kuleta wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kutumia fursa nyingi zinazopatikana nchini.
Mwisho.